22 wafariki kwa kuporomokewa na kifusi mgodini Simiyu
14 January 2024, 12:42 pm
Tumefanikiwa kuokoa miili ishirini na mbili ya wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika mgodi wa Ikinabushu kufuatia kuporomoka kwa duara wakati wakiendelea na shughuli za uchimbaji
Na,Daniel Manyanga
Watu ishirini na mbili wamefariki dunia kwa kufukiwa (kuporomokewa) na kifusi kwenye machimbo ya madini ya dhahabu yaliyopo katika kijiji cha Ikinabushu kata ya Gilya wilayani Bariadi mkaoni Simiyu wakiwa ndani ya duara.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Simiyu INSP.Faustine Mtitu akiwa eneo la tukio amesema kuwa tukio hilo limetokea mnamo tarehe 13.01.2024 majira ya saa kumi na moja alfajiri katika mgodi huo wa Ikinabushu uliopo kata ya Gilya huku chanzo cha vifo hivyo kikiwa ni ardhi kuporomoka kutokana na kulowana kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani hapo.
INSP.Mtitu ameongeza kuwa zoezi la uokoaji kupitia jeshi la Zimamoto la uokoaji kwa ushirikiano na Wachimbaji wadogo mgodini hapo lilianza mara moja baada ya kupata taarifa ambapo hadi wanasitisha zoezi la uokoaji mnamo majira ya saa mbili na nusu usiku walifanikiwa kutoa miili 22 ya Wachimbaji wadogo wa dhahabu na yote ni ya kiume.
“Wachimbaji waliingia kwenyea duara bila kufuata utaratibu wa migodini maana kila mchimbaji anapoingia kwenye duara lazima aweze kujiorodhesha kwenye daftari ili kuwa rahisi kujuwa ameingia muda gani maana kwenye duara kuna oksijeni ndogo”Amesema Mtitu
“Mpaka majira ya saa mbili na nusu usiku ambapo zoezi tunalisitisha tulifanikiwa kuokoa miili 22 hivyo leo tumekuja kuhakiki kama kuna miili mingine ambayo ilibakia lakini hakuna hata mwili mmoja na kubaki idadi ile ile hivyo niwapongeze sana Waandishi wa habari kwa kuendelea kuujuza umma juu ya tukio hili bila kusahau Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Wachimbaji wadogo kwa kuweza kufanikisha zoezi zima kuanzia jana”Amesema Mtitu
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt.Yahaya Nawanda ,amesema kuwa tukio hilo ni la kwanza kutokea mkoani hapo kuua watu wengi kiasi hicho na kuacha simanzi kubwa kwa wahanga ambapo kamati ya ulinzi na usalama mkoani hapo imesitisha shughuli za uchimbaji katika mgodi huo mpaka pale watakapojiridhisha kama ni salama kwa wachimbaji kuendelea na shughuli hizo.
Taarifa za awali kutoka kwa wasimamizi wa mgodi huo zimeeleza kuwa shughuli za uchumbaji zilisitishwa kutokana na kupewa ushauri kutoka kwa wakaguzi wa mgodi huo lakini baadhi ya wachimbaji walikaadi agizo hilo na kuingia kinyemera na kuanza kuchimba mnano majira ya usiku wa manane.