18 wagundulika na kipindupindu Maswa, mmoja afariki dunia
1 November 2023, 11:52 am
Na Nicholaus Machunda
Watu 18 wamegundulika na ugonjwa wa kipindupindu wilayani Maswa mkoani Simiyu huku mmoja akifariki dunia kutokana na ugonjwa huo.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Bi, Salma Mahizi wakati akitoa elimu juu ya uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu na namna ya kuchukua tahadhari kupitia Radio Sibuka fm.
Bi Mahizi amesema kuwa wagonjwa wa kwanza kugundulika walitokea kijiji cha Sayusayu kilichopo kata ya Buchambi ambapo hadi sasa zaidi ya wagonjwa 18 wamegundulika na kati ya hao mmoja amefariki dunia.
Amesema ugonjwa wa kipindupindu ni hatari ambapo baadhi ya dailili zake ni pamoja na kuharisha na kutapika hali inayopelekea mwili kuchoka na kukosa nguvu na hatimae kifo.
Aidha mratibu huyo amesema kuwa halmashauri imeweka mikakati madhubuti ili kuhakikisha mlipuko huo wa kipindupindu unadhibitiwa usiendelee kuenea katika maeneo mengine pamoja na kuimarisha sehemu za huduma za afya.