Mfumo wa mlipakodi kidijitali kurahisisha upatikanaji namba mlipa kodi mkoani Simiyu
22 June 2023, 6:50 pm
Na, Alex Sayi
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Simiyu imesema kuwa tangu kuanzishwa kwa huduma ya mlango kwa mlipa kodi (Taxpayer Portal) imerahisisha upatikanaji wa namba ya mlipa kodi (TIN) kwa wananchi.
Akizungumza na Sibuka Fm Benjamini John Afisa Elimu na Huduma (TRA) mkoa wa Simiyu amesema kuwa huduma hiyo ya kimtandao imewapunguzia usumbufu wananchi kwani kwa sasa huhitaji kupanga mstari (foleni) ofisi za (TRA) kupata (TIN).
John amesema kuwa kumekuwa na ongezeko la walipa kodi mkoani Simiyu kutokana na wepesi na urahisi uliopo kwa sasa kwa wafanyabiasha wa kupata (TIN) kwa njia ya simu za mkononi yaani simu janja.
Ameongeza kuwa elimu wanayotoa kwa mlipa kodi kwa njia ya matangazo, midahalo,semina, vipindi vya radio, kupita mlango kwa mlango imesaidia kukuza uelewa kwa wananchi na kuongeza idadi ya walipa kodi wapya.
Lucius Theonesti, meneja (TRA) wilayani Maswa alisema kuwa ulipaji kodi kwa hiari unaipunguzia gharama mamlaka hiyo ya ukusanyaji wa mapato huku akiwaomba baadhi ya wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi na kufunga biashara zao waone umuhumu wa kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Diwani wa kata ya Jijabirishi wilayani hapa Daudi Lubinza alizungumzia suala la baadhi ya wafanyabiashara katani kwake kudaiwa kukwepa kulipa kodi kwa kufunga biashara zao, alisema kuwa suala hilo kwa sasa halipo kutokana na elimu inayoendelea kutolewa na mamlaka hiyo.