Sibuka FM

RC NAWANDA ATOA SIKU SABA KUKAMILISHA MIUNDOMBINU YA MILANGO KITUO CHA AFYA SHISHIYU..

16 December 2022, 8:00 pm

Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt.Yahaya  Nawanda  ametoa siku saba (wiki moja) kwa uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Maswa  kuweka milango mingine imara katika kituo cha afya cha Shishiyu kufuatia iliyokuwa imewekwa kutokidhi ubora.

Dkt.Nawanda akiwa katika ziara yake ya kikazi ya siku tatu wilayani hapo ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa  na fedha nyingi za walipakodi wazalendo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na toshelevu.

Ambapo akiwa katika kata ya Shishiyu alipata nafasi ya kukagua kituo cha afya cha Shishiyu na kukutana na madudu katika kituo hicho “Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassani hapa ametoa kiasi cha fedha milioni 500 ili kujenga kituoa cha afya hichi ili kuondoa adha ya wananchi kufuata huduma umbali mrefu lakini nashangaa kuna baadhii ya watu wanafanya mchezo mchafu wa kuhujumu miundombinu hii” Amesema Dkt.Nawanda Rc Simiyu.

“Mkuu wa wilaya natoa  siku saba  milango iwe imeshawekwa ambayo ni imara tofauti na hii ambayo imewekwa tu bila kuangalia ubora maana haiwezekani kituo hichi tu waweke milango chini ya kiwango  wakati katika wilaya zingine walipewa wote pesa sawa na hapa lakini wao wameweka milango yenye ubora lazima hapa kuna kitu” Amesema Rc Simiyu Dkt.Nawanda.

Katika hatua nyingine Dkt.Nawanda ametoa kiasi cha milioni moja katika kuwaunga mkono wananchi wa kata hiyo kukamilisha jingo la maabara katika kituo hicho ili kianze kutoa huduma .

Awali mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge amemuomba mkuu wa mkuu wa mkoa Dkt.Nawanda  kuwahimiza wananchi wa kijijini hapo kuchangia ujenzi huo ili kuweza kukamilisha  sehemu ambazo bado hazijakamilika ili kituo kianze kufanya kazi kwa wakati.

“Mkuu wa mkoa kwanza nikushukuru kwa kujitolea kiasi cha milioni moja lakini pia nikuombe tuungane kwa pamoja kuwahamasisha wananchi wa kijijini hapo kuchangia miradi ya maendeleo inayotekelezwa sisemi kwamba hawachangii wanachangia sana lakini bado kunamwamko mdogo sana kwa wananchi kuchangia miradi hii” Amesema Dc Maswa,Aswege Kaminyoge.