TANROAD simamieni kwa ukaribu ujenzi wa miundombinu ya barabara
6 November 2021, 4:58 pm
Na mwandishi wetu Daniel Manyanga,Simiyu
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, David Kafulila amemtaka wakala wa barabara TANROAD mkoani hapo kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara ili kubaini mapungufu mapema na kuepusha gharama zaidi za ukarabati.
David Kafulila ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua ukarabati wa barabara ya kiwango cha lami ya Maswa kwenda Mwigumbi yenye urefu wa kilomita 50.3 ambapo baadhi ya maeneo yenye urefu wa kilomita 3.6 upande wa Simiyu yalionekana kujengwa chini ya kiwango kinachotakiwa.
Ameongeza kuwa wakala wa barabara TANROAD mkoani hapo kuwa pamoja na kufanya vizuri katika usimamizi wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara bado kuna haja ya kufuatilia kwa ukaribu wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo ili kujuwa mapungufu yatakayoepusha gharama zaidi za ukarabati.
Mhandisi John Mkumbo ni meneja wa TANROAD mkoa wa Simiyu amesema kuwa ujenzi huo ulikamilika kwa asilimia 100 baada ya TANROAD kufanya uchunguzi na kubaini kilomita 10 kujengwa chini ya kiwango kwa Simiyu km 3.6 na Shinyanga Zaidi km 5 lakini mpaka sasa mkandarasi wa kampuni ya CHICO kutoka China anatakiwa kurudia km 15 ambapo zimebainika kuwa chini ya kiwango huku tayari mkandarasi ameshalipwa kiasi cha shilingi billion 69.
Kwa upande wake mhandisi mshauri wa mradi huo kutoka kampuni ya KYONG DONG ya nchini Korea Kusini, Mazige H Self amesema kuwa matumizi ya udongo mbovu uliopelekea barabara hiyo kujengwa chini ya kiwango huku akimhakikishia mkuu wa mkoa wa Simiyu ,David Kafulila kuwa matatizo yaliyojitokeza mwanzo hayatajirudia tena.
Katika hatua nyingine mkuu wa mkoa wa Simiyu ,David Kafulila ameahidi kumsaidia mtumishi mstaafu kuunganishiwa umeme ambapo mpaka sasa ni mwaka wa tatu hajaunganishiwa umeme pamoja na kwamba ameshalipia gharama za kuwekewa umeme.