Pangani FM

Wakufunzi 10 kubadili vyombo vya habari kijinsia

17 March 2023, 3:08 pm

Mwezeshaji kutoka Shirika la UZIKWASA Bi.Salvata Kalanga. Picha na Erick Mallya

Na Erick Mallya

Shirika la UZIKWASA lililopo wilayani Pangani Mkoani Tanga kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limehitimisha  mafunzo maalumu ya siku 4 yaliyowakutanisha viongozi waandamizi wa vyombo vya Habari vya Tanzania bara na visiwani.

Baadhi ya wakufunzi hao wakijadili katika moja ya mafunzo hayo.

Viongozi hao ambao idadi yao ni 10 wamepatiwa mafunzo ya wakufunzi (ToTs) ili kuwapa mbinu mbalimbali za kuwawezesha wengine kwenye vituo vyao katika Kuimarisha utangazaji wa jinsia ndani na kupitia vyombo vya Habari.

Kulia mshiriki kutoka Uyui FM Bw. Ibrahim pamoja na Bi Zania Kweka kutoka Dodoma FM.

Mafunzo hayo yamefanyika  katika moja ya Kumbi za mikutano za Royal Village zilizopo jijini Dodoma kuanzia Jumatatu Machi 13 hadi 16, 2023.

Anthony Masai kutoka Tripple A, ya Arusha akichangia hoja katika mafunzo hayo.

Wakizungumza mara baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo washiriki hao wametoa shukrani zao kwenda kwa Shirika la UZIKWASA kutokana na mbnu za Kiuongozi walizozipata.

Nawashukuru sana kwa mafunzo haya ambayo yana mbinu wezeshi zilizonisaidia kujiona na kujitafakari, wakati nafikiria safari yangu ya uongozi nimegundua kuwa nimesababsisha maumivu

Zania Kweka wa Dodoma FM

Sauti za wakufunzi hao mara baada ya kuhitimishwa kwa mafunzo hayo ya Siku 4.

Kwa miaka mingi Shirika la UZIKWASA limekuwa likitoa mafunzo ya ‘mguso’ ambayo yamekuwa yakiwawezesha watu binafsi kutafakari nafasi zao katika kuchochea mabadiliko chanya pamoja na mabadiliko ya kitaasisi na Jamii kwa ujumla.

Mshauri wa masuala ya vyombo vya Habari Bi. Lillian Urio  kutoka Dar es Salaam akizungumza wakati wa mjadala wa masuala ya Jinsia ndani ya vyombo vya Habari. Picha na Erick Mallya

Wanufaika wa mafunzo hayo wamekuwa vongozi wa dini, viongozi wa taasisi, waandishi wa habari, vongozi wa kisiasa na wale wanaosimamia masuala ya Jinsia na Mazingira.

Faida za mafunzo hayo zimetambulika katika ngazi ya Kitaifa na Kimataifa.