Umbali wa sekondari wa km 24,Wananchi wajenga madarasa manne kupunguza safari ya kufuata masomo
11 January 2023, 12:27 pm
Na mwandishi wetu, Daniel Manayanga
Zaidi ya Millioni thelatheni ambayo ni michango ya wananchi,mfuko wa jimbo la Maswa Magharibi zimeshatumika katika ujenzi wa Shule ya Sekondari Sayusayu iliyopo Kata ya Buchambi Wilayani Maswa Mkoani Simiyu ili kupunguza adha wa wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata masomo.
Ujenzi huo umekuja kufuatia adha ya wanafunzi wa Sekondari waliokua wanalazimika kutembea umbali wa kilomita zaidi ya (12) kwenda na kurudi kufuata masomo katika shule ya sekondari Kinamwigulu.
“Wananchi wa Sayusayu waliamua kuchangia wao wenyewe bila kushurutishwa na mtu yeyote na kuanza kujenga haya madarasa manne,ofisi mbili na choo lengo ni kuwanusuru watoto wao kufuata masomo umbali mrefu” amesema kaimu afisa mtendaji wa kata ya Buchambi,Yohana Simba.
“Wanafunzi wengi wanaofaulu kuendelea na masomo ya Sekondari kijijini hapa wamekuwa hawamalizi masomo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kujiunga na makundi ya hovyo,mimba za utotoni na utoro sugu unachangiwa na umbali wa shule ya sekondari”amesema kaimu afisa mtendaji kata ,Yohana Simba.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa kijiji cha Sayusayu wamesema kuwa Shule hiyo imechelewa kukamiliika kwa wakati kutokana na changamoto za usimamizi kuwa mbovu kutoka kwa mwenyekiti wa kijiji hivyo.
“Kuchelewa kukamilika kwa shule hii kulichangiwa na usimamizi mbovu kutoka kwa mwenyekiti wa kijiji hichi ambaye amehusika sana katika ubadhilifu wa michango ya wananchi ambapo katika utawala wake hatujawahi hata siku moja kukaa kikao cha kusomewa mapato ya michango ya wananchi” amesema Raphael Makunde.
“Wananchi wamechangia sana hii shule zaidi ya mara tatu lakini hatuoni hatua yoyote ya ujenzi pesa za michango ya wananchi inawanufaisha watu wachache” amesema Japhet Jisena.
“Mbunge ameshatoa pesa mara mbili mara ya kwanza alitoa katika shule ya Sekondari Sayusayu lakini idara ya fedha na mipango fedha hiyo iliihamishia katika shule ya Sekondary Kinamwigulu kwa ajili ya kufanya kazi huko” amesema diwani kata ya Buchambi Slyvanus Mipawa.
“Fedha ya mara pili mbunge alitoa ambayo ilinunua mabati na kufanikisha kuezekwa lakini changamoto kubwa manunuzi yalifanyika bila ya kamati ya ujenzi kushirikishwa na mpaka sasa kuna kiongozi ambaye hadi hajawasilisha michango ya wananchi na anatafutwa” amesema diwani kata ya Buchambi,Slyvanus Mipawa.
“Ukiangalia michango ya wananchi katika ujenzi huu hata milioni nne hazifiki lakini nashangaa sana kuja kusikia kuwa mimi nimekula michango ya wananchi zaidi ya milioni 19 hali ambayo siyo kweli “amesema mwenyekiti anayetuhumiwa kula michango ya wananchi,Konda James
“Asilimia kubwa Shule hii kufika hapa ni michango ya mbunge ambapo mpaka sasa ameshatoa zaidi ya milioni 14 na siyo 19 kama wanavyosema wananchi kuwa nimekula ,na shule nilianzisha mimi kumshawishi hata mbunge” Konda James