Asilimia 40% ya vifo vya Watoto nchini vinatokana na watoto kuzaliwa Njiti.
26 September 2021, 11:15 am
Imeelezwa kuwa asilimia Arobaini ya vifo vya Watoto nchini vinatokana na watoto kuzaliwa kabla ya siku zao (Njiti).
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na maendeleo ya Jamii na Mbunge wa Jimbo la Maswa mashariki Stanslaus Nyongo wakati akipokea vifaa vya kuhudumia watoto njiti vilivyotolewa na Taasisi ya DORIS MOLLEL FOUNDATION katika Ukumbi wa Halmashauri wilayani Maswa, Mkoani Simiyu.
Mh Nyongo amesema kuwa tatizo la watoto njiti linatatulika endapo watapewa huduma bora na kuondoa unyanyapaa na mila potofu kwa jamii zikiamini kuzaliwa mtoto njiti kwenye familia ni kupata laana na mikosi inayoweza kujitokeza kwenye familia husika..
Amesema kuwa mara nyingi kumekuwa na changamoto kubwa katika kuwalea watoto wa namna hiyo hali ambayo imekuwa ikipelekea baadhi ya akina mama kutoroka hospitali wakikwepa gharama na usumbufu wa namna ya kuwalea watoto hao..
Akikabidhi Msaada wa vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni Hamsini Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Tasisi ya Doris Mollel Foundation Bi. Doris Mollel ambaye pia yeye alizaliwa mtoto njiti amesema ameguswa na mahitaji ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati huku akielezea ushuhuda wake wa kuzaliwa njiti…
Aidha mganga mkuu wa Wilaya ya Maswa Dr Adorat Mpollo amesema kuwa changamoto hiyo ipo ambapo wastani wa watoto Ishirini na tano wanaozaliwa kwa mwezi katika Hospitali ya Maswa kati yao nusu ni njitikati.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi wilaya ya Maswa Mhandisi Paul Jidayi amesema kuwa anawashukuru sana Taasisi ya Doris Mollel Foundation kwa kukuswa na kusaidia watoto wa wilaya ya Maswa ambao wamekuwa wakipoteza Maisha kutokana na changamoto ya kuzaliwa njiti…
Baadhi ya wazazi wa watoto njiti wamezungumza na Sibuka fm na kuishukuru Serikali kwa msaada huo kwani wamekuwa wakipata changamoto ya kuwalea na kuwatunza watoto ambao wamekuwa wakizaliwa kabla ya wakati….
Hapa chini ni Picha mbalimbali za mapokezi ya vifaa kwa ajili ya watoto Njiti