Katibu wa Amcos ya Kidema wilayani Maswa matatani
1 August 2024, 5:13 pm
Mwendesha Mashtaka wa Takukuru ameeleza kuwa Mshtakiwa alifikishwa Mahakamani hapo Januari 05, 2023 kwa Makosa Mawili ya kutoa fedha kiasi Tsh. 1,228,000/= kwenye akaunti ya KIDEMA AMCOS na kuzitumia kwa matumizi yake binafsi badala ya kulipa ushuru kwenye akaunti ya chama kikuu Cha Ushirika Mkoa wa Simiyu SIMCU
Na Nicholaus Machunda – Simiyu
Mahakama ya Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu imemhukumu adhabu ya kifungo Cha miaka 15 jela aliyekuwa Katibu wa AMCOS ya Kidema Wilaya ya Maswa Bw Richard Bundala Nchemba baada ya kukutwa na hatia katika makosa mawili
Kosa la kwanza ni Ufujaji na Ubadhirifu kinyume na Kifungu cha 28(2) Cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura 329 Marejeo ya Mwaka 2019 kikisomwa pamoja na aya ya 21 jedwali la kwanza pamoja na vifungu vya 57(1) na 60 (2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura 200 Marejeo ya mwaka 2019.
Kosa la pili ni Wizi kwa Wakala kinyume na Kifungu cha 265 na 273(b) vya Sheria ya Kanuni za adhabu Sura 16 Marejeo ya Mwaka 2019.
Hukumu hiyo imetolewa Julai 30, 2024 kutokana na shauri la Uhujumu Uchumi Na. 1/2023 lililokuwa katika Mahakama ya Wilaya Maswa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Enos Misana chini ya Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU Wilayani Maswa Bw. Bahati Madoshi.
Aidha Mwendesha Mashitaka wa Takukuru ameeleza kuwa Mshtakiwa alifikishwa Mahakamani hapo Januari 05, 2023 kwa Mashtaka tajwa hapo juu kwa kutoa fedha kiasi Tsh. 1,228,000/= kwenye akaunti ya KIDEMA AMCOS na kuzitumia kwa matumizi yake binafsi badala ya kulipa ushuru kwenye akaunti ya chama kikuu Cha Ushirika Mkoa wa Simiyu SIMCU
Kwa Upande wa Mshitakiwa baada ya kupewa nafasi ya kujitetea alisema kwamba baada ya kutoa Fedha hizo Benki kwenye Akaunti ya KIDEMA AMCOS ghafla alivamiwa na Oporation Mananger wa Kampuni ya Birchad na kunyang’anywa Fedha hizo Hata hivyo alipotakiwa kuithibitishia Mahakama kuhusu Utetezi huo alishindwa ndipo Mahakama ikamtia Hatiani ili iwe fundisho kwa Watu wengine wenye tabia hizo zinazodumaza Uchumi wa Taifa