DC Kaminyoge: Elimu ya Kisheria iendelee kutolewa kwa Wananchi
1 February 2024, 8:09 pm
Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu Mhe, Aswege Kaminyoge amewataka wadau wa Sheria kuendelea kutoa Elimu kwa Wananchi kwani wanawategemea sana katika Utoaji wa Haki.
Hayo ameyasema katika kilele cha Wiki ya Sheria katika Viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Maswa na Kusema kuwa kila kiongozi akitimiza wajibu wake Wananchi watakuwa na Furaha na kuona Mahakama ndio kimbilio la kupatikana haki ya kila Mtu.
Mh Kaminyoge amesema kuwa Serikali ina viongozi ngazi zote lengo kuu ni kumsaidia Mhe, Rais katika majukumu ya kuwatumikia wananchi na kuhakikisha wanapata huduma zote za msingi na Mazingira wezeshi.
Akitoa Hotuba ya kilele cha Wiki ya sheria, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Maswa Mh, Enos Misana amesema kuwa Mahakama ndio chombo pekee cha Utoaji wa Haki kikatiba kwa kuongozwa na Dira yake.
Mh Misana ameongeza kuwa katika wiki ya sheria wamekuwa na jukumu la kuelimisha Wananchi kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo sheria, shughuli za Kimahakama, kupokea maoni na Mapendekezo ya wananchi.
Kwa Upande wake Mwendesha Mashitaka Wilaya ya Maswa Mhe, Suzani Masule amesema kuwa Mahakama pekee haiwezi kutoa haki bila kushirikisha Wadau wengine wanahusika katika Utoaji wa Haki.