Wananchi wapewa mbinu za kukabiliana na Tembo vamizi.
11 May 2021, 1:24 pm
Wananchi wilayani Meatu Mkoani Simiyu wameaswa kushirikiana na wataalamu wa Wanyama pori ili kudhibiti Uharibifu unaofanywa na wanyama katika maeneo yanayozungukwa na Hifadhi za wanyama.
Wito huo umetolewa na mwakilishi wa Mkurugenzi idara ya Wanyama Pori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Ndugu Pellage Kauzeni wakati akihitimisha mafunzo ya Vijana thelathini kutoka wilaya tatu za mkoa wa simiyu zinazopakana na Hifadhi za Wanyama..
Kaimu Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyapori –TAWIRI Bi Janemary Ntalwila amesema kuwa vijana hao thelathini wamefundishwa mbinu za kukabiliana na wanyama waharibifu hasa wanyama hao wanapovamia kwenye mashamba ya Wananchi.
Aidha Mkuu wa wilaya ya Meatu Ndugu Joseph Chilongani na mkuu wa Wilaya ya Bariadi Ndugu Festo Kiswaga Wakasema kuwa Mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka kwani yatajibu Hitaji la wananchi juu ya kupambana na wanyama waharibifu hivyo Serikali iwawezeshe vitendea kazi..
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi wilaya ya Meatu mkoani Simiyu Juma Chazenga Mwiburi amesema kuwa wataalamu hao wa Wanyapori wamefanya jambo zuri hasa kuwaelimisha walengwa wenyewe ambao ni wananchi kwani itasaidia kudhibiti tembo hao ambao wamekuwa wakivamia mashamba mara kwa mara.