DC Maswa: Wananchi tunzeni vyanzo vya maji
16 December 2023, 12:01 pm
Wadau wa maji na Wananchi watakiwa kutunza vyanzo vya maji ili kuweza kukabiliana na ukame unaosababishwa na shughuli za kijamii pamoja na mabadiliko ya tabia nchi
Na Daniel Manyanga
Mkuu wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu Mhe.Aswege Kaminyoge amewataka Wananchi na Wadau wa Sekta ya Maji Wilayani hapo kutunza vyanzo vya Maji Ili kukabiliana na ukame unaosababishwa na shughuli za kijamii pamoja na Mabadiliko ya tabia nchi.
Kaminyoge ametoa Rai hiyo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Mwaka wa Wadau wa Sekta ya Maji ulioandaliwa na wakala wa Maji na usafi wa Mazingira Vijijini Wilayani hapo (RUWASA) uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya hiyo.
Kaminyoge amesema kuwa kumekuwepo na tabia za baadhi ya watu kufanya shughuli za kijamii katika vyanzo vya Maji hali ambayo inapelekea Kuua vyanzo hivyo hasa mto Sola unaotegemewa kujaza bwawa la New Sola ambalo ni Chanzo Kikuu Cha Maji mjini hapo na kuwaomba wadau wa maji kuendelea na zoezi la upandaji wa miti, kuacha shughuli za kijamii katika vyanzo hali ambayo itasaidia kutunza vyanzo vya maji wilayani hapo.
Kaminyoge ameongeza kuwa Kuna baadhi ya Viongozi wa kisiasa na Wananchi wamekuwa ni sehemu ya kuhujumu miundombinu ya maji ambayo tayari inafanya kazi hivyo amewataka kuachana na tabia hizo na badala yake Wadau wa Maji,Viongozi na Wananchi wawe sehemu ya kulinda miundombinu hiyo ili iweze kunufaisha hata vizazi vijavyo.
Awali meneja wa RUWASA wilaya ya Maswa Mhandisi.Lukas Madaha amesema kuwa kuanzia mwaka 2019 mwezi Julai wametekeleza miradi mbalimbali ya Maji yenye jumla ya fedha zaidi bilioni 8 hali ambayo imepelekea kuongeza upatikanaji wa maji vijijini hadi kufikia asilimia 74.
Betty Isaack ni Mratibu wa shirika lisilokuwa la kiserikali la World Vision Mradi wa Shishiyu AP Amesema kuwa World Vision kama Mdau muhimu wa Maji wamechimba visima virefu vitatu katika mradi wa World Vision Shishiyu unaonufaisha wananchi zaidi ya elfu nne na mwaka wa fedha 2023/24 wamepanga kutumia zaidi ya milioni mia moja na thelathini kusambaza maji katika vitongoji na vijiji ambavyo havikuweza kupata maji kwa awamu iliyopita katika kata ya Shishiyu.