Sibuka FM

Katibu wa Amcos ya Kidema wilayani  Maswa matatani

1 August 2024, 5:13 pm

Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu

Mwendesha Mashtaka wa Takukuru  ameeleza  kuwa  Mshtakiwa  alifikishwa Mahakamani hapo Januari 05, 2023 kwa  Makosa Mawili ya kutoa fedha kiasi Tsh. 1,228,000/= kwenye akaunti ya KIDEMA AMCOS na kuzitumia kwa matumizi yake binafsi badala ya kulipa ushuru kwenye akaunti ya chama kikuu Cha Ushirika  Mkoa wa Simiyu SIMCU

Na Nicholaus Machunda – Simiyu

Mahakama   ya  Wilaya  ya  Maswa  Mkoani  Simiyu  imemhukumu  adhabu ya kifungo Cha miaka 15  jela aliyekuwa Katibu wa AMCOS ya  Kidema  Wilaya ya Maswa   Bw  Richard  Bundala   Nchemba   baada ya kukutwa na  hatia  katika makosa  mawili

 Kosa la kwanza ni Ufujaji  na Ubadhirifu kinyume na Kifungu cha 28(2) Cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa  Sura 329 Marejeo ya Mwaka 2019  kikisomwa pamoja na aya ya 21 jedwali la kwanza pamoja na vifungu vya 57(1) na 60 (2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura 200 Marejeo ya mwaka 2019.

 Kosa la pili ni Wizi kwa Wakala kinyume na Kifungu cha 265 na 273(b)  vya Sheria ya Kanuni za adhabu  Sura 16 Marejeo ya Mwaka  2019.

Hukumu  hiyo  imetolewa  Julai 30, 2024 kutokana na shauri la Uhujumu Uchumi  Na. 1/2023 lililokuwa katika Mahakama ya Wilaya Maswa  mbele ya Hakimu  Mkazi Mfawidhi   Enos Misana chini ya  Mwendesha  Mashtaka  kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU Wilayani  Maswa  Bw.  Bahati Madoshi.

Aidha  Mwendesha Mashitaka  wa  Takukuru   ameeleza  kuwa  Mshtakiwa  alifikishwa Mahakamani hapo Januari 05, 2023 kwa  Mashtaka tajwa hapo juu kwa kutoa fedha kiasi Tsh. 1,228,000/= kwenye akaunti ya KIDEMA AMCOS na kuzitumia kwa matumizi yake binafsi badala ya kulipa ushuru kwenye akaunti ya chama kikuu Cha Ushirika  Mkoa wa Simiyu SIMCU

Kwa  Upande  wa  Mshitakiwa  baada  ya  kupewa  nafasi  ya  kujitetea  alisema  kwamba   baada  ya  kutoa  Fedha  hizo    Benki  kwenye  Akaunti  ya   KIDEMA  AMCOS   ghafla  alivamiwa   na  Oporation Mananger  wa  Kampuni  ya  Birchad na  kunyang’anywa  Fedha   hizo Hata  hivyo  alipotakiwa  kuithibitishia   Mahakama   kuhusu  Utetezi  huo   alishindwa   ndipo  Mahakama  ikamtia  Hatiani  ili  iwe  fundisho  kwa  Watu  wengine  wenye  tabia   hizo  zinazodumaza  Uchumi  wa  Taifa