Sibuka FM

Mboje wa Singida atupwa jela miaka 30,faini ya laki tatu kwa kubaka Maswa

12 June 2024, 4:20 pm

Pichani ni muonekano wa jengo la mahakama ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu Picha na Daniel Manyanga

Ukatili wa kijinsia umetajwa vyanzo vya matatizo ya kisakolojia kwa wahanga hivyo sheria ziwe na makali kwa mtuhumiwa hali ambayo itaweza kupunguza au kumaliza ukatili.”

Na, Daniel Manyanga 

Mahakama  ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imemhukumu, Mboje Paul (28) mkazi wa kijiji cha Ipuya mkoa wa Singida kwenda jela miaka 30 na kulipa faini ya shilingi 300,000/= kwa  kosa la kubaka.

Mbele ya hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Maswa,Mhe.Azizi Khamis,Mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya mashitaka ya Taifa wilayani hapo mkaguzi msaidizi wa polisi ,Vedastus Wajanga amesema kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo mwezi wa November 2023 mnamo majira ya saa 6:00 mchana katika kijiji cha Budekwa wilayani hapo.

Mwendesha mashitaka huyo ameendelea kuiambia  mahakama kuwa mshitakiwa alimbaka muhanga ambaye jina lake limehifadhiwa kwa kumlaghai kuwa atampa pesa  na baada yakufanya kitendo hicho mshtakiwa alimpa muhanga kiasi cha pesa shilingi 1000/= kwa ahadi kuwa asiende kumwambia dada yake ambaye anaishi naye nyumbani hapo.

Mwendesha mashitaka kutoka ofisi ya mashitaka ya Taifa wilayani hapo,Vedastus Wajanga amesema kuwa kosa hilo ni kinyume na  kifungu cha130 (1)(2)(e) na 131 (1) cha  sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022 .

 Wajanga amesema kuwa taarifa zilifika kituo cha polisi wilaya ya Maswa ambapo mshitakiwa alikamatwa na alipohojiwa katika kituo hicho  alikataa kabisa kufanya kitendo hicho na baada ya upelelezi kukamilika mshitakiwa alifikishwa mahakamani kwa hatua zingine za kisheria ambapo upande wa mashitaka ulileta mashahidi watano na kielelezo kimoja ili kuthibitisha kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo na baada ya ushahidi huo kutolewa mshitakiwa naye alipewa nafasi ya kuwasilisha utetezi wake.

Mara baada ya utetezi huo Kukamilika mahakama hiyo ilimtia hatia mshitakiwa huyo na mwendesha mashitaka aliiomba mahakama kumpatia adhabu kali mshitakiwa ili iwe funzo kwake na jamii kwani makosa ya kubaka yanaongezeka katika jamii na yanaleta athari kubwa kwa muhanga kisakolojia,kijamii,kiuchumi , kiafya pia makosa kama haya ni ukatili wa kijinsia katika jamii na hatimaye  kusababisha maradhi au kifo kwa muhanga

Akitoa hukumu hiyo iliyotolewa  Juni 10 mwaka huu na hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama hiyo, Mhe.Azizi Khamis  mara baada ya kusikiliza utetezi wa pande zote mbili za mshitakiwa na Jamhuri bila kuacha mashaka yoyote ndipo mahakama ilimhukumu kwenda kutumikia kifungo cha miaka 30 jela na kulipa fidia kiasi cha fedha laki tatu kwa muhanga kwa kosa la kubaka