Itilima wakosa huduma ya maji safi na salama kwa wiki tatu
16 April 2024, 7:32 pm
Watembea umbali wa kilomita 3 kufuata huduma ya maji safi na salama kufuatia mota ya kusukuma maji kuungua kijijini hapo.
Na. Daniel Manyanga
Wananchi wa vijiji vya Mlimani na Zanzui vilivyopo wilayani Itilima mkoani Simiyu wakosa huduma ya maji safi na salama ya bomba kwa muda wa wiki tatu kufuatia mota ya kusukuma maji kuungua hatua iliyopelekea kupata huduma hiyo kijiji jirani cha Kabale kilichopo umbali wa kilomita tatu kutoka kwenye vijiji hivyo.
Akizungumza na Sibuka Fm ilipofika kijijini hapo kwa lengo la kujionea adha wanayopitia hivi sasa, wananchi hao mwenyekiti wa kijiji cha Zanzui Ndg. Michael Mabula amesema kuwa kuungua kwa mota hiyo ambayo husukuma maji katika vijiji hivyo wananchi wamepata changamoto kubwa hali ambayo imewafanya kupata huduma ya maji safi na salama kutoka kijiji kingine kilichopo umbali wa kilomita 3.
Kwa upande wake meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira vijijini RUWASA wilaya ya Itilima Hussein Yahaya amesema kuwa tayari wameshachukua hatua za kurejesha huduma hiyo muhimu kwa wananchi katika maeneo hayo.