TARURA kutumia zaidi bil. 4.1 ukarabati wa miundombinu Maswa
21 March 2024, 7:05 pm
Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA)Wilayani Maswa Mkoani Simiyu wanatarajia kuzifanyia marekebisho Barabara zenye mtandao wa Km,227.21 zilizoathiriwa na Mvua za msimu.
Na. Alex Sayi
Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) imeendelea na matengenezo ya barabara zilizoathiriwa na mvua za msimu kwa lengo la kurejesha mawasiliano kwa Wananchi.
Hayo yamesemwa na Mhandisi wa barabara wilayani hapa Baraka Libungo kwa niaba ya Meneja (TARURA) Wilaya na kusema kuwa kwa sasa wamefikia (40%) ya matengenezo hayo.
Libungo ameongeza kuwa matengenezo hayo yanagharimu zaidi ya Tsh. bil 4.1 kwa kujumisha shughuli za ujenzi wa madaraja, mitaro, kuweka karavati, ujenzi wa kingo za madaraja, kuchonga na kuweka moramu kwenye mtandao wa barabara wenye urefu wa Km. 227.21.
Peter Mlyandingu Diwani wa kata ya Nguliguli wilayani hapa ameishukuru serikali kwa kuwa sikivu chini ya Meneja (TARURA) kwa kunusuru kwa wakati uharibifu wa miundombinu hiyo.
Sayi Shola na Kija Samweli wakazi wa kijiji cha Mwashegeshi kata ya Ngulinguli wilayani hapa kwa nyakati tofauti wamezungumzia hali ya uharibifu wa daraja la Mwashegeshi na kusema kuwa inahatarisha usalama wa watumiaji huku akiiomba (TARURA) kuharakisha ujenzi wa daraja hilo