96 wahitimu mafunzo ya udereva Maswa
1 March 2024, 8:07 pm
Jumla ya maafisa usafirishaji 96 wamepatiwa vyeti vya udereva na leseni za uendeshaji vyombo vya moto ikiwemo pikipiki na magari madogo baada ya kufuzu mafunzo ya uendeshaji wa vyombo hivyo.
Akikadhi vyeti hivyo na leseni , Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mh Aswege Kaminyoge amesema kuwa alitoa nafasi hiyo ya kupata mafunzo bure ya uendeshaji wa vyombo vya Moto ili kupunguza ajali zisizo za lazima.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya ametoa miezi Mitatu kwa Maafisa Usafirishaji ambao hawajapata Mafunzo wahakikishe wanapata Mafunzo na kupata Leseni itayomfanya afanye shughuli zake bila kusumbuliwa na Askari wa Usalama barabarani.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa chuo cha Ufundi Stadi Binza Mabula Daniel amesema kuwa Wamefundisha mambo mbalimbali ikiwemo alama na Michoro ya Barabarani, Udereva wa Kijihami na Sheria za Usalama Barabarani
Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Simiyu SSP Namsemba Mwakatobe amewataka waendesha vyombo vya Moto waliopata Mafunzo kwenda kuwa Mabalozi kwa Wengine kwenda kusoma ili kupunguza ajali za barabarani.
Yusuph Mahega ni Mwenyekiti wa Waendesha Boda boda Wilaya ya Maswa amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kutoa Mafunzo bure kwa maafisa hao huku wakimuomba asichoke kuendelea kuwasaidia.