Maswa:Wanawake bado niwaathiria wa vitendo vya ukatili wakijinsia.
11 December 2023, 6:56 pm
Takwimu zimeonyesha kuwa bado kuna idadi kubwa ya wanawake wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia Wilayani Maswa Mkoani Simiyu.
Na Alex Sayi.
Imebainishwa kuwa Wanawake Wilayani Maswa Mkoani Simiyu wameendelea kuwa waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa mujibu wa Takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Ustawi wa Jamii Wilayani hapa.
Hayo yamesemwa na Afisa Ustawi wa Jamii Wilayani hapa Grace Mmasi kwenye kilele cha maadhimisho ya siku (16) za kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika Desemba 10 Mwaka huu viwanja vya Madeko Wilayani hapa kwa ufadhili wa Shirika la World Divission
Mmasi amesema kuwa kwa mujibu wa Takwimu kuanzia mwezi Januari hadi Octoba mwaka huu wanawake wapatao (626)walifanyiwa ukatili wa kijinsia Wilayani Maswa Mkoani hapa.
Akizungumzia suala la ukatili wa kijinsia Mkuu wa kituo cha Polisi Wilayani Maswa Mkoani hapa (ASP) Mkimbu Ramadhani amesema kuwa idadi kubwa ya waathirika wa Ukatili wa kijinsia ni wanawake
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya Maswa Dkt,Hadija Zegega akizungumzia athari zinazotokana na masuala ya ukatili wa kijinsia amesema kuwa uwepo wa vitendo hivyo unawaathiri wahusika kisaikologia,kijamii na kiuchumi.
Nae Mratibu wa Mradi wa maendeleo ya Jamii Kata ya Shishiyu Wilayani hapa Betty Isaack amesema kuwa Miradi inayotekelezwa na Shirika la World Divission Wilayani hapa imelenga kuleta usawa kwenye maeneo yasiyo na usawa.
Aidha kwa upande wake mgeni rasmi Venance Saria Afisa Tarafa Tarafa ya Nung’hu Wilayani hapa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya amesema kuwa jamii inapaswa kuwekeza kupinga ukatili wa kijinsia bila kubagua jinsia ya mtu.