Madiwani Maswa wakerwa na majibu ya TARURA
19 November 2023, 4:37 pm
TARURA wilayani Maswa mkoani Simiyu inayohudumia mtandao wa barabara wenye jumla ya Km 184.2 na iliyofikia 77% ya Barabara zinazopitika kwa nyakati zote za msimu sawa na km 837.39 imelalamikiwa kwakushindwa kupeleka kwa wakati wakandarasi kwenye baadhi ya Barabara Wilayani hapa.
Na Alex Sayi
Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA)Wilayani Maswa Mkoani Simiyu umelalamikiwa na baadhi ya Madiwani kwa kushindwa kupeleka wakandarasi kwenye baadhi ya Barabara korofi kwa zaidi ya miaka (10) sasa.
Hayo yamesemwa na baadhi ya Madiwani hao kwenye Baraza la Madiwani lililoketi Nov 17 Mwaka huu kwenye ukumbi wa Halmashauri, huku baadhi ya Madiwani hao wakionekana kusikitishwa na majibu ya ubabaishaji yaliyokuwa yakitolewa na Mwakilishi wa Meneja (TARURA) Wilayani hapa.
Perus Makalwe Diwani wa Viti maalumu amesema kuwa licha ya taarifa kufika Ofisi za (TARURA)kwa zaidi ya miaka (10)kuhusiana na Barabara ya Mwakaleka,Bugalama,Bugolola bado (TARURA)wameshindwa kufanyia kazi suala hilo.
Stiven Dwese Diwani wa Kata ya G’wigwa Wilayani hapa amesema kuwa baadhi ya Barabara zilizochongwa na kuwekewa molamu zimeanza kukatika kutokana na Mvua chache zinazonyesha hivyo kuwaomba (TARURA) kuimarisha ubora wa Barabara hizo
Sadick Duttu Diwani wa Kata ya Senani Wilayani Maswa Mkoani hapa alitaka kujua nini kinasababisha wakandarasi kushindwa kufika site kwa wakati licha ya fedha kutengwa kwa muda mrefu
Paulo Maige Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Wilayani hapa alisema kuwa itapendeza ikiwa (TARURA)watakuwa na majibu yauhakika na sio kutoa majibu ya kubabaisha mbele ya Baraza hilo,Maige alisema hayo baada ya msemaji wa (TARURA) kushindwa kuwa na majibu sahihi kwa swali lilioulizwa na Diwani wa Kata ya G’wingwa Stiven Dwese kuhusiana na Barabara ya Sola,Sakasaka Mwandoya.