DC Maswa aonya wanaohujumu miundombinu ya maji
16 November 2023, 8:22 pm
Na Nicholaus Machunda
Mkuu wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu Mh, Aswege Kaminyoge ameonya wananchi wanaohujumu miundombinu ya maji yanayotoka Ziwa Viktoria kuja kata ya Sengwa iliyopo wilayani hapa kupitia wilaya ya Kishapu.
Mh Kaminyoge amesema hayo wakati Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ilipotembelea mradi huo ambao umekuwa ukihujumiwa mara kwa mara na wananchi kwa kupasua bomba la maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu na kunyweshea mifugo yao..
Aidha Mh Kaminyoge amesema kuwa tayari ameshachukua hatua ya kuwasiliana na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu ili kuweka namna nzuri ya wananchi hao kujengewa vituo vya kichotea maji na kunyweshea vifugo yako ili wasiendelee kuharibu miundombinu hiyo.
Akitoa taarifa ya Utekelezaji wa Mradi huo Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) Wilaya ya Maswa Mhandisi Lucas Madaha amesema kuwa kumekuwepo na adha ya Wananchi wa Sengwa kukosa maji kutokana na kutobolewa kwa bomba hilo..
Mhandisi Madaha ameongeza kuwa katika mwaka wa Fedha Ujao RUWASA imepanga kuongeza mtandao wa Maji ili vijiji vyote vya kata ya Sengwa vipate huduma ya Maji ya kutoka ziwa viktoria.
Baadhi ya Wananchi wa kijiji hicho Wameishukuru Serika kwakuwaletea mradi huo huku wakiiomba Serikali kuwachukulia hatua Wananchi wanaohujumu Miundo mbinu ya maji hali inayopelekea wananchi wengi kukosa maji.