Kamati ya bunge yaridhishwa mradi hatimiliki Maswa
13 November 2023, 4:58 pm
Mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi vijijini unaotekelezwa na halmashauri ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu unatarajia kutoa hatimiliki 100,000 kwa wananchi.
Na Alex Sayi
Kamati ya kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii imeridhika na utekelezaji wa mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi vijijini unaotekelezwa na halmashauri ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Timothy Mzava (Mb) jimbo la Korogwe Vijijini mkoani Tanga wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mwadila kata ya Sukuma eilayani hapa kwenye mkutano wa hadhara.
Mzava ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo utasaidia kuondoa migogoro kati ya kijiji na kijiji, shamba na shamba, kiwanja na kiwanja na kuongeza thamani ya ardhi na kuwasaidia wananchi kuboresha maisha yao.
Geophrey Mizengo Pinda Naibu Waziri wa Ardhi , Nyumba Maendeleo na Makazi amesema kuwa wilaya ya Maswa ni miongoni mwa wilaya 7 za awali zinazonufaika na utekelezaji wa mradi huo ikiwemo Mufindi, Songwe, Mbinga, Chamwino, Longido na Tanganyika.
Vivian Christian amesema kuwa mradi unatekelezwa kwa muda wa miaka mitano 2022-2027 kwa wilaya ya Maswa na mradi ulianza Feb, 2023 hadi kufikia Novemba 10/2023 mradi umetumia Sh.Mil 819.
Ibrahim Jagadi mkazi wa Mwadila akizungumza na Sibuka Fm amesema kuwa wanaishukuru serikali kwa kuwapatia hatimiliki bure kwa kuwa awali upatikanaji wa hati hizo ilikuwa ni gharama kubwa na usumbufu ulikuwa ni mkubwa mno.
Sahani Dwese akizungumza na Sibuka Fm amesema kuwa upimaji wa maeneo unasaidia kuondoa migogoro kwenye makazi na mipaka ya mashamba kwa kuwa kila mtu anakuwa anajua eneo lake linaishia wapi.