Mwashegeshi wamkataa afisa mtendaji wa kijiji
6 October 2023, 7:30 am
Maafisa watendaji wa kata wilayani Maswa wametakiwa kuitisha vikao vya vitongoji, vijiji na kata vilivyopo kisheria ili kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Na Alex Sayi Maswa Simiyu
Wananchi na wakazi wa kijiji cha Mwashegeshi kata ya Nguliguli wamemuomba mkuu wa wilaya ya Maswa Aswege Kaminyoge kuondoka na afisa mtendaji wa kijiji hicho Debora Mwansela kwa kuwa amekuwa kero kwao.
Hayo yamesemwa na wananchi hao kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kiwanja cha mpira shule ya msingi Mwashegeshi katani hapo wakati wakitoa kero na malalamiko yao kwa mkuu wa wilaya hiyo.
Kauli hiyo imesemwa na Yakobo Petro Jidai ambaye ni mwenyekiti wa tawi (CCM) wakati akizungumzia kero ya afisa mtendaji huyo wa kijiji na namna anavyokwamisha shughuli za maendeleo kijijini hapo.
Awali diwani wa kata hiyo ya Ngulinguli wilayani Maswa Mh. Peter Mlyandingu akifungua mkutano huo amewaomba wananchi wajenge tabia ya kuhudhuria mikutano ili waweze kutoa kero zao.
Mkuu wa wilaya hiyo Aswege Kaminyoge ameutaka uongozi wa halmashauri ndani ya siku 30 kuhakikisha wanaweka utaratibu wa kuwashirikisha wananchi kimamilifu kupitia vikao halali vya kisheria.
Akizungumza na Sibuka Fm afisa mtendaji wa kijiji hicho kuhusiana na tuhuma za wananchi kumlalamikia kuwa hakai kituoni na amekuwa kikwazo cha maendeleo ya kijiji hicho, Debora Mwansele amesema kuwa tuhuma hizo hazina ukweli kwa kuwa hakuwa kituoni hapo kwa sababu maalum.