Takukuru Simiyu yaokoa milioni 500 za mfanyabiashara
18 August 2023, 10:05 am
TAKUKURU mkoa wa Simiyu imeokoa mamilioni ya fedha za mfanyabiashara ambaye mali zake zingepigwa mnada kwa bei ya kutupwa.
Na Nicholaus Machunda
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini TAKUKURU mkoa wa Simiyu imefanikiwa kudhibiti upotevu wa zaidi ya Shilingi milioni mia tatu katika mnada haramu wa ghala na nyumba tatu za kuishi mali ya mfanyabiashara anayejulikana kwa jina la Sibu Nsugi Manabu mkazi wa wilaya ya Bariadi mkoani hapa.
Akitoa taarifa ya robo ya nne ya mwaka wa fedha 2022/2023 ( April – Juni ) kwa waandishi wa habari, Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Simiyu Aron Misanga amesema kuwa thamani ya ghala hilo ni zaidi ya Shilingi milioni mia tano lakini lilikusudiwa kuuzwa chini ya shilingi milioni mia mbili.
Naibu Mkuu wa Takukuru huyo amefafanua kuwa mfanyabiashara huyo alikopa fedha kwenye benki na kushindwa kurejesha hivyo kupelekea mali zake kukamatwa na kutaka kuuzwa kwa mnada wa hadhara ulioendeshwa na kampuni ya Bani Investment Limited hali ambayo utaratibu haukufuatwa na kupelekea Takukuru kuingilia kati.
Katika hatua nyingine Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Simiyu imefuatilia Miradi Ishirini na tano (25) ya Maendeleo yenye thamani ya Zaidi ya Shilingi Bilioni 6. 8 katika Sekta za Elimu, Afya, Maji na Barabara kwa lengo la Kudhibiti Ubadhilifu wa Fedha za Umma.
Aidha TAKUKURU Mkoa wa Simyu inaendelea na Mikakati ya Kuzuia Rushwa katika Eneo la Ukusanyaji wa Mapato kwa kutoa Elimu kwa makundi mbalimbali rasmi na yasiyo rasmi, Sehemu zenye mikusanyiko ya Watu pamoja na Vipindi vya Radio Jamii Sibuka fm.