Maswa: Wafugaji waaswa kushiriki utunzaji mazingira, vyanzo vya maji
15 August 2023, 3:30 pm
Wafugaji Wilayani Maswa Mkoani Simiyu watakiwa wawe sehemu ya uhifadhi wa mazingira na utunzaji wa vyanzo vya Maji.
Na,Alex Sayi.
Wafugaji Wilayani Maswa Mkoani Simiyu wameaswa kushiriki utunzaji wa Mazingira na vyanzo vya Maji kwa kutokupeleka mifugo kwenye chanzo kikuu cha Maji cha Bwawa la New Sola kinachotegemewa na wakazi Wilayani hapa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Maswa Aswege Kaminyoge wakati akizungumza na baadhi ya wafugaji katika kijiji na Kata ya Zanzui Wilayani hapa ili kubaini changamoto zinazowakabili wafugaji hao.
Mayenga Sangalali mfugaji na mkazi wa Zanzui Wilayani hapa amesema kuwa wafugaji walishindwa kuendelea kunywesha mifugo yao kwenye mabirika kutokana na gharama kuwa kubwa.
Msimamizi wa moja ya mabirika katani hapa toka Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (MAUWASA)amesema kuwa wafugaji walishindwa kulipia Sh.40 kwa kila kichwa cha Ng’ombe.
Kaminyoge akitolea ufafanuzi wa gharama za unyweshaji kwenye mabirika hayo amesema kuwa wameshawasiliana na (Ewura) na wamekubaliana kushusha bei hiyo hadi Sh.20
Diwani wa Kata hiyo Jeremia Shigala Makondeko amesema kuwa anamshukuru Rais Samia kwakuendelea kuwasogezea huduma za kijamii wananchi wa Kata hiyo huku akiwaasa wafugaji wa Kata hiyo kujenga desturi ya kupanda miti ya mbao na matunda ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya Nchi.