Maswa: Wajane waaswa kuchangamkia fursa 10% mikopo ya halmashauri
28 June 2023, 7:01 pm
Kwenye picha ni mkuu wa wilaya ya Maswa Mhe. Aswege Kaminyoge aliyesimama akizungumza na baadhi ya akina mama wajane walioshiriki maadhimisho ya wajane wilayani hapo kwenye ukumbi wa mikutano
Na Mwandishi,Alex.F.Sayi
WANAWAKE Wajane wilayani Maswa mkoani Simiyu wameaswa kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na halmashauri hiyo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kujikwamua kiuchumi.
Kauli hiyo imebainishwa na mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Aswege Kaminyoge kwenye maadhimisho ya siku ya Wajane Duniani, iliyofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo Juni mwaka huu huku kaulimbiu ikiwa ni “Wezesha Wajane kwa Teknolojia Bora; kuwainua kiuchumi”.
Kaminyoge amesema kuwa serikli kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto za wajane kwa kuimarisha mifumo ya kulinda haki za wajane kwa kutungwa sheria za msaada wa kisheria No.1 ya Mwaka 2017.
“Serikali imeanzisha msaada wa kisheria unaowezesha makundi maalum ikiwemo wajane na watoto kupata haki zao, kutekelezwa kwa kampeni ya kisheria ya Mama Samia na kampeni ya Mwanamke na Ardhi, zimechochea afua na kukuza haki ya upatikanaji wa msaada wa sheria.” Amesema Kaminyoge.
Kaminyoge ameongeza kuwa kupitia kampeni ya Sheria ya Mama Samia, jumla ya wanawake 1,896,012 na wanaume 1,369,910 walifikiwa na kupatiwa elimu ya msaada wa kisheria na haki za kibinadamu kwa mikoa yote Tanzania bara.
David Ntinginya, ni mwanasheria wa halmashauri ya wilaya amesema kuwa serikali imewezesha kutungwa kwa Sheria ya Ardhi ya Kijiji Namba 5(1999) kifungu cha 20(1) ambacho kinatoa nafasi kwa wanawake wakiwemo wajane kumiliki ardhi.
“Halmashauri imejipanga kuhakikisha Wajane wanapata msaada wa kisheria bure,ili wasidhurumiwe Haki zao na leo wameanzisha Shirikisho la Wajane huu utakuwa ni mwanzo wakuwafikia Wajane wote na kupata taarifa zao kwa usahihi,Shirikisho litawasaidia Wajane kujiona sio Wajane.”Amesema Ntinginya.
Mkuu wa Divission ya Maendeleo ya Jamii Wilayani hapa Rodgers Lyimo amesema kuwa maadhimisho hayo yamewakutanisha zaidi ya Wajane 400 kutoka maeneo tofauti tofauti Wilayani hapa huku Wilaya hiyo ikikadria kuwa kuna zaidi ya Wajane 8,000 Wilayani humo.
Lyimo amesema kuwa maadhimisho hayo yamewasaidia Wajane Wilayani hapo kuzijua Sheria zinazowalinda Wajane hao dhidi ya dhuruma za kimirathi pindi wanapoondokewa na wenzi wao,huku Wajane hao wakishauriwa kuzitumia fursa za kisheria kupata haki zao.
Mwenyekiti Mteule wa shirikisho la Wajane Wilaya Carloline Shayo amesema kuwa wajane wamefurahi kukutana na wanasheria ambao wanatambua haki za wajane nakuongeza kuwa shirikisho hilo linaanza mianzo mipya ya wajane kukutana na kutatua changamoto zao.
“Naomba niwaase kinamama tusimame kwenye zamu zetu hasa kipindi hiki ambapo maadili yanamomonyoka wakati watoto wanalawitiwa tusiteteleke,familia ni Mama,Mama akisimama familia inasimama na tuendelee kuwaombea watoto wetu na kuwalinda usiku na mchana.”Amesema Shayo.
Shayo ameongeza kuwa Ujane unachangamoto nyingi unapokuwa mjane unafungua ukurasa mpya wa maisha utapoteza marafiki,Ndugu na hata majirani wote watakutenga wakiamini kuwa ukiwa karibu yao utakuwa tegemezi kwao.
Jackline Jibunge Mjane mkazi wa Unyanyembe Kata ya Sola Wilayani hapa amesema kuwa elimu waliyoipata itakuwa chachu kwa wengine kwakuwa wamejifunza namna ya kupata haki zao na hatua za kufuata pale mjane anapofiwa na mwenzi wake.