DC Maswa awataka wananchi kupisha mradi wa umeme
28 April 2023, 7:33 am
Alex F. Sayi
Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu Mhe. Aswege Kaminyoge amewataka wakazi Wilayani hapo wanaopitiwa na Mradi wa umeme toka Ibadakuli Mkoani Shinyanga hadi Bariadi Simiyu wenye msongo wa Kilovoti 220 kuachia maeneo yao kwaajili ya utekelezaji wa Mradi huo.
Kaminyoge amesema hayo wakati akizungumza na watendaji wa Vijiji,Kata na baadhi ya wamiliki wa maeneo kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa.
Akizungumzia Mradi huo unaotarajiwa kutekelezwa ndani ya miaka miwili kuanzia Aprili mwaka huu,utakao gharimu kiasi cha zaidi ya Sh. Bil 48.7 Mkuu huyo wa Wilaya amewaomba wamililki wa maeneo kuwatayari kuruhusu kuanza kwa shughuli za awali za Mradi huo kabla ya malipo yao.
“Ninawaomba wamiliki wa maeneo mniamini mruhusu shughuli za awali za utekelezaji wa Mradi huu ziendelee na kunawataalamu watapita kwenye maeneo yenu kuchukua sampuli za udongo kupeleka maabara najua bado hamjalipwa ila ndani ya miezi miwili mtakuwa mmelipwa stahiki zenu.”Amesema Kaminyoge.
Elen Nyanza, Mkazi wa Malita Wilayani hapo akichangia maoni yake kwenye mkutano huo amesema kuwa siku zote wanyonge hawana haki kwakuwa kinachoendelea kwa sasa itakuwa kinyume na mkataba tulioingia na watekelezaji wa Mradi huo .
“Mkataba ilikuwa tulipwe ndani ya miezi 6 hadi sasa tunazaidi ya miezi 8 hatujalipwa na sasa mnasema tupishe maeneo Mradi unaanze baada ya miezi miwili tutalipwa kweli mnyonge atakuwa mwananchi kwenye hii Nchi maana nikama mnatulazimisha kutoa maeneo yetu.”Amesema Nyanza.
Viviani Mkamba Mkuu wa Idara ya Ardhi Wilayani hapo amesema kuwa wakazi wapatao 434 waishio kwenye Vijiji kumi na tano wanaopitiwa na Mradi huo wanatarajiwa kulipwa fidia ya maeneo yao na zoezi la uhakiki linaendelea kwenye maeneo hayo.
“Wakazi wa Vijiji vya Malita, Zanzui, Mwashegeshi, G’hami, Mwabomba, Mondo, Hinduki, Mwang’huhi, Matalambuli, Chuli, Busamuda, Isulilo, Njiapanda na Wigelekelo ndio watao lipwa fidia ya maeneo yao.”Alisema Viviani.
Changamoto ya umeme kukatika mara kwa mara mkoani Simiyu imekuwa inaleta hasara kubwa kwa wafanayabiasha hasa wa viwanda kwani inawagharimu kutumia njia mbadala ili kuendesha mitambo ya viwandani ambapo inachukua fedha nyingi kuendesha shughuli za uzalishaji viwandani ambapo kukamilika kwa mradi huo utawapunguzia adha ya kukatika kwa umeme mkoani hapo.