Mkurugenzi Halmashauri ya Meatu amwamuru Mkandarasi kubomoa Msingi aliojenga chini ya Kiwango..
8 November 2022, 8:52 am
SIMIYU: Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu Msoleni Dakawa, ameamuru kubomolewa kwa msingi wa madarasa manne, uliokuwa unaendelea kujengwa katika Shule ya Sekondari Sakasaka iliyopo wilayani hapo baada ya kubaini umejengwa chini ya kiwango.
Aidha Mkurugenzi huyo amemwagiza Fundi aliyekuwa anajenga msingi huo kubomoa na kuanza kuujenga upya kwa gharama zake mwenyewe na kwa kufuata taratibu zote zinazotakiwa kwenye ramani ya ujenzi (BOQ).
Akiwa kwenye zoezi kukagua madarasa yote yanayojengwa kwa ajili kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023, Mkurugenzi huyo amefika shuleni hapo na kubaini fundi alitumia nondo mbili badala ya nne kwenye mzunguko wote wa msingi jambo ambalo ni hatari.
Madhaifu mengine ni fundi huyo kuchimba msingi huo kwa vipimo ambavyo siyo sahihi, ambapo vipimo sahihi msingi unatakiwa kuwa na kina cha sentimeta 75 hadi 90, upana setimeta 69 na mita 9 kwa urefu wa darasa moja ambapo fundi huyo hakufanya hivyo.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo alibaini kuwa fundi huyo hakuwa amemwaga mchanga wa awali chini ya msingi na hakuwa amemwaga zege ya awali kabla ya kuweka tofali, huku ikibainika tatizo kubwa ni kamati za ujenzi kutotimiza wajibu wake..