Maswa:Mauwasa kutumia milioni 500 kusambaza maji safi na salama mjini Maswa.
7 March 2022, 7:38 pm
Na mwandishi,Daniel Manyanga,Simiyu
Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa(Mauwasa) mkoani Simiyu imekusudia kutumia kiasi cha Sh 509,884,320 katika kukamilisha mradi wa usambazaji wa maji mjini humo.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa, Mhandisi Nandi Mathias mbele ya waandishi wa habari waliotembelea mjini hapo kwa lengo kujionea utekelezaji wa mradi huo.
Mhandisi Nandi amesema kuwa mradi huo unajulikana kama Uboreshaji Huduma ya Maji Maswa Mjini kwa Ustawi wa Taifa kwa Maendeleo katika kupambana na Maambukizi ya Uviko 19 na kuongeza kuwa kazi zilizopangwa kutekelezwa kwenye mradi huo ni pamoja na Uchimbaji wa mtaro , kulaza bomba na kufikia urefu wa Kilomita 21.65,Ujenzi wa Vituo vine vya kuchotea maji na Ujenzi wa chemba 10.
Mhandisi Nandi amesema hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 74 ya utekelezaji wake na unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu na utaongeza wigo wa Mamlaka hiyo kupata wateja wapya 1000 na kunufaisha mitaa 10 ya mjini Maswa na vijij vitatu ambapo ameitaja mitaa hiyo ni Pamoja na Mitimirefu,Majengo,SolaMwabomba,SolaUnyanyembe,Uzunguni,Ujenzi,Jashimba,Ikungulyasubi,Majebele na Badabada .
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge amewataka wananchi kuitunza miradi hiyo sambamba na kutunza miundombinu ya maji na kuonya mtu yeyote ambaye atabainika kuihujumu atachukuliwa hatua kali za kisheria.