Simiyu:serikali ya mkoa wa Simiyu kufufua viwanda viwili vya pamba
21 February 2022, 3:47 pm
Na mwandishi,Daniel Manyanga,Simiyu
Serikali mkoani Simiyu inatarajia kufufua viwanda viwili ambavyo vilijengwa wakati wa ukoloni lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi hususani wakulima wa zao la pamba kupata huduma na soko la karibu.
Hayo yameelezwa na mkuu wa mkoa wa Simiyu David kafulila wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali wilayani Maswa mkoani hapo na kuongeza kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya rais Mhe.Samia Suluhu Hassan imedhamilia kuwakomboa wakulima wa pamba nchini.
Kafulila amesema kuwa wanaenda kufufua viwanda viwili kiwanda kimoja ni kwa ajili ya kukamua mafuta ya pamba cha “Lugulu ginnery” kilichopo wilayani Itilima na cha pili ni “Sola ginnery” kilichopo wilayani Maswa ambacho hiki kitakuwa cha kuchambua pamba na tayari serikali ya awamu ya sita imeshatoa maelekezo ya kufufuliwa kwa viwanda hivyo.
Kafulila ameongeza kuwa serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania chini ya rais Mhe.Samia Suluhu Hassan haitaki ujanja ujanja kwenye pamba na itaendelea kushughulika na wale wote wanaohujumu ushirika hapa nchini.
Awali akisoma taarifa kwa niaba ya meneja wa chama kikuu cha ushirika(SIMCU) wilaya ya Maswa afisa ushirika wilayani hapo Cosmas Budodi amesema kuwa kiwanda hicho “Sola ginnery” cha kuchambua pamba kilijengwa na waasia na kikaanza kufanya kazi kipindi cha ukoloni mnamo mwaka 1958 na badae kununuliwa kutoka kwa waasia kwenda kwa Victoria federation kisha kukabidhiwa rasmi mnamo mwaka 1959 na badae kukabidhiwa katika chama kikuu cha ushirika mkoa wa Simiyu(SIMCU) mnamo mwaka 2021 kufuatia kuanzishwa kwa mkoa wa Simiyu.
Aidha Budodi ameiomba serikali kusaidia utatuzi wa baadhi ya changamoto zinazokikabili kiwanda hicho ili kusaidia uendeshaji wa shughuli pindi kitakapoanza kufanya kazi katika msimu huu wa pamba.
Katika hatua nyingine Davida Kafulila amelidhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa tanki la kusambazia maji wilayani hapo lenye ujazo wa lita milioni moja ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 80.