IDADI YA WAJAWAZITO WANAOJIFUNGULIA KWENYE VITUO VYA AFYA YAFIKIA ASILIMIA 96% WILAYANI MASWA.
26 January 2022, 7:56 pm
Idadi ya akina mama wanaojifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya wilayani Maswa Mkoani Simiyu imeongezeka kutoka Asilimia 55 kwa Mwezi Januar -June, 2021 hadi kufikia Asilimia 96.4% kwa Mwezi Julai –Decemba, 2021 huku hamna kifo kitokanacho na Uzazi ikilinganishwa na mwezi Januari-June, 2021 kukiwa na vifo 5 vitokanavyo na uzazi…
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Huduma ya Afya ya Baba Mama na Mtoto wilayani Maswa Dr Angella Ngaiza wakati akitoa Elimu kupitia Radio Sibuka fm juu Umuhimu wa akina Mama kujifungulia kwenye vituo vya Afya kwani inasaidia kupunguza vifo vitokanavyo na Uzazi..
Dr Ngaiza amesema kuwa pamoja na ongezeko hilo wapo akina mama wajawazito wachache ambao hawajapata mwamko hivyo kupelekea baadhi yao kujifungulia njiani wakati wanaenda kwenye vituo vya Afya jambo linalohatarisha Maisha ya mama Mjamzito.
Aidha amesema mafanikio hayo yamekuja kwa ushirikiano wa watoa huduma za Afya, Wadau mbalimbali wa Afya na Jamii kwa ujumla hivyo waendelee kuwahamasisha akina mama wajawazito kwenda kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma kwani ni salama zaidi ukilinganisha za kujifungulia nyumbani..
Picha za Mratibu wa Huduma ya Afya ya Baba, Mama na Mtoto wilayani Maswa akiwa studio za Sibuka fm akitoa Elimu ya Afya ya Uzazi.