mwalimu mkuu mikononi mwa polisi kwa udanganyifu wa mitihani ya darasa la nne
2 November 2021, 1:58 pm
Na mwandishi wetu Daniel Manyanga,Bariadi
Mwalimu mkuu shule ya msingi Shimbale katika halmashauri ya Bariadi mkoani Simiyu Gaudensia Anyango mwenye umri wa miaka 45 Mjaruo na mkazi wa mtaa Shimbale anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kufanya udanganyifu katika mitihani ya darasa la nne iliyofanyika tarehe 28 na 29 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari kaimu Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Simiyu kamishina msaidizi wa polisi Shadrack .M. Masiji amesema kuwa mwalimu huyo aliwachukua wanafunzi wa darasa la tano na la sita kwa ajili ya kuwafanyia mitihani ya darasa la nne wanafunzi wenzao 23 ambao ni watoro katika shule hiyo .
Masiji amesema kuwa wizara ya TAMISEMI imekuwa na utaratibu wa kuzipatia motisha shule ambazo zinafanya vizuri katika mitihani hivyo kulikuwa na uwezekano wa mwalimu huyo alifanya hivyo ili kufaulisha wanafunzi wote .
ACP Masiji ameongeza kuwa tayari mtuhumiwa ameshakamatwa na yupo kituo cha polisi mjini Bariadi akiendelea kuhojiwa kuhusiana na tuhuma hizo na mara baada ya upelelezi huo kukamilika jalada litafikishwa ofisi ya taifa ya mashtaka kwa hatua za kisheria ili kufikishwa mahakamani.
Aidha jeshi la polisi mkoa wa Simiyu limetoa wito kwa watumishi wote wanaohusika na zoezi la usimamizi wa mitihani ya kidato cha Pili na kidato cha Nne kuacha mara moja vitendo vyovyote vya udanganyifu katika mitihani inayoendelea kwani kamati za mitihani za wilaya na mkoa kwa kushirikiana na jeshi la polisi halitafumbia macho suala hilo la udanganyifu katika mitihani hiyo.