Ugonjwa wa akili wapelekea kujinja watoto wake wawili kisha naye kujichinja.
22 October 2021, 8:14 pm
Na mwandishi wetu Daniel Manyanga,Simiyu.
Mama mmoja aitwaye Ng’washi Makigo mwenye umri miaka 35 Msukuma na mkazi wa kijiji Gula wilayani Maswa mkoani Simiyu amewaua watoto wake wawili kwa kuwachinja kwa kutumia kisu kisha naye kijichinja.
Kamanda wa polisi mkoa wa Simiyu ACP Blasius Chatanda akizungumza na waandishi wa Habari mkoani hapo amesema kuwa tukio hilo limetokea mnamo tarehe 22/10/2021 majira ya saa 8:30 asubuhi katika kitongoji cha Mwatambuka kijiji na kata ya Lalago wilayani Maswa mkoani Simiyu ambapo mama huyo alitekeleza tukio hilo ndani ya nyumba ya Luja Makigo.
ACP Chatanda amewataja watoto hao ni Nseya Kisena miaka 7, na Majaba Kisena mwenye umri wa mwaka 1 na miezi 5, ambapo walikutwa wameuwa kwa kuchinjwa na kisu huku uchunguzi wa awali umeonesha kuwa mama huyo ambaye pia ni marehemu ndiye aliyetekeleza tukio hilo la mauwaji kwa watoto wake kwa kuanza kumchinja mtoto wake mkubwa wa kike Nseya Kisena na kisha kumchinja mtoto wake mdogo wa kiume Majaba Kisena na hatimaye kijichinja yeye hadi kufa.
Miili yote ya marehemu hao imekutwa ndani ya chumba kimoja cha Luja Makigo huku kisu kinachosadikika kutumika katika kutekekeleza mauaji hayo kikiwa kimebaki shingoni kwenye mwili wa mama huyo huku chanzo cha tukio kikitajwa kuwa ni ugonjwa wa akili, kwani mdogo wa marehemu huyo Luja Makigo ameeleza kuwa dada yake amekuwa akisumbuliwa na tatizo hilo la ugonjwa wa akili kwa muda mrefu na huko nyuma miaka kadhaa iliyopita alishawahi kufanya jaribio la kujiua kwa kujichana shingoni kwa kutumia kiwembe.
Kwa upande wa wake Luja Makigo ambaye ni mdogo wa marehemu na mwenyeji wa marehemu hao amesema alibaini tukio hilo mara baada ya kurudi akitokea zahanati ya kijiji cha Gula alipokwenda kwa ajili ya kupata matibabu.
ACP Chatanda amesema jeshi la polisi mkoa wa Simiyu linatoa wito kwa wananchi kuongeza umakini dhidi ya watu ambao wanasumbuliwa na matatizo ya akili ili kuepuka kuleta madhara kwa jamii.
Halikadhalika ACP Chatanda amesema kuwa hali ya usalama mkoa wa Simiyu ni shwari na hii ni kutokana na jitihada za jeshi la polisi kwa kushirikiana na wananchi pamoja na vyombo vingine vya usalama katika kuzuia uhalifu na kupambana na wahalifu.