mkoa wa simiyu na mkakati wa kuzalisha tani laki tano za pamba msimu wa kilimo 2021/2021
12 October 2021, 9:44 am
Mkuu wa mkoa wa Simiyu David Kafulila amewaomba wadau mbalimbali wa zao la pamba mkoa hapo kuhakikisha mkakati wa zao hilo wa kuzalisha tani laki tano za pamba unatekelezwa kwa vitendo na siyo kwa makaratasi lengo nikuongeza thamani ya zao hilo Pamoja na kuiwezesha Tanzania kuwa kinara wa zao la pamba barani Afrika na hatimaye kuingia kumi bora duniani.
David Kafulila ameyasema hayo wakati wa kikao cha wadau mbalimbali wa kilimo cha pamba cha tathimini kilichofanyika wilayani Meatu na kuongeza kuwa ili kufikia malengo ya mkoa ya kuzalisha tani laki tano lazima kila mdau wa pamba kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Juma Topera ni katibu tawala msaidizi uchumi na uwezeshaji mkoa wa Simiyu amesema kuwa katika kuhakikisha nchi ya Tanzania inakuwa kinara wa uzalishaji wa pamba barani afrika kuna sababu ya mkoa huo kufanya kilimo chenye tija.
Naye mkuu wa wilaya hiyo Fauzia Hamidu amezitaja changamoto walizokutana nazo kipindi cha kutoa elimu ya uhamasishaji kuwa ni pamoja na baadhi ya jamii kudai uhaba wa samadi kutokana na kutokuwa na ng’ombe wa kutosha sambamba na uwepo wa tembo katika maeneo yao hatua inayopelekea kukatishwa tamaa.
Kwa upande wake afisa kilimo kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa huo Kija Kayenze ametaja baadhi ya mikakati kuwa ni pamoja na kufanya uhamasishaji kupitia mikutano ya hadhara,kupokea maelekezo kutoka ngazi ya mkoa hadi ngazi ya kijiji , kujadili na kufanya tathimini kila baada ya wiki mbili .
Mkoa wa Simiyu unazalisha nusu ya pamba yote nchini huku wilaya ya Meatu ikitajwa kuongoza kwa uzalishaji kwa wilaya zote nchini.