Waziri Mashimba Ndaki akabidhi Komputa kwa shule za Sekondari jimboni kwake.
16 September 2021, 4:02 pm
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka Wakuu wote wa shule za sekondari katika jimbo la Maswa Magharibi Mkoani Simiyu kuanzisha madarasa ya kompyuta ili wanafunzi kupata maarifa zaidi.
Waziri Ndaki ambaye pia ni Mbunge wa jimbo hilo amesema hayo wakati akikabidhi kompyuta 10 na printa 2 kwa shule ya sekondari Buchambi na shule ya sekondari Badi zilizoko wilayani hapa ambapo kila shule ilipata kompyuta 5 na printa moja.
Amesema kuwa lengo la serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu ni kuhakikisha inawajengea uwezo wanafunzi wa shule za sekondari kwa ajili ya somo la tehama ili kuendana na kasi na mabadiliko ya kiteknolojia.
Aidha amewataka walimu wa shule hizo ambazo wamekabidhiwa vifaa hivyo kuvitunza na kuhakikisha viko salama ili viweze kuwanufaisha wanafunzi katika masomo yao.
Vifaa hivyo vilivyokabidhiwa vyenye thamani ya sh Milioni 23.1 vimetolewa na serikali kupitia mfuko wa mawasilino kwa wote vitakuwa ni mkombozi kwa walimu pamoja na wanafunzi katika kusaidia suala zima la teknolojia pamoja na mawasiliano.