Jumla ya Vijiji 45 vya Wilaya ya Maswa kunufaika na TASAF awamu ya Tatu kipindi cha Pili.
28 May 2021, 11:30 am
Jumla ya vijiji Arobaini na tano vilivyopo Wilayani Maswa Mkoani Simiyu vinatarajiwa kunufaika na Mfuko wa maendeleo ya Jamii i – TASAF kwa awamu ya tatu kipindi cha Pili.
Hayo yameelezwa na Mratibu wa TASAF wilaya ya Maswa Bi, Grace Tungaraza wakati wa kikao kazi cha Kuwajengea uelewa juu ya Utambuzi na Uandikishaji wa kaya masikini katika vijiji vilivyokuwa havipo katika Mpango huo.
Deocles Leopord ni Mwakilishi wa mkurugenzi mtendaji wa TASAF makao makuu amesema kuwa katika kipindi cha kwanza awamu ya tatu maeneo mengi hayakufikiwa hivyo katika kipindi hiki cha pili kila kijiji kitafikiwa na walengwa kutambuliwa.
Aidha ndugu Leopord amefafanua zaidi kuhusu walengwa na wanufaika wa mpango huu wa kunusuru kaya masikini – TASAF na Kumshukuru Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa kwa kukubali kutoa wataalamu ambao wataenda kutekeleza zoezi hilo la kubaini kaya masikini.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Maswa ambae alikuwa mgeni rasmi katika Mafunzo hayo ya utekelezaji Mh, Aswege Kaminyoge amesema kuwa elimu itolewe ya kutosha namna ambavyo walengwa watapatikana ili kuondoa malalamiko yanayojitokeza kwa wananchi na kuongeza kuwa awamu hii imezingatia changamoto zilizojitokeza katika awamu zilizopita.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Maswa Mh, Paul Maige kwa niaba ya Madiwani wenzake ameishukuru serikali kwa kuja na mpango wa kunusuru kaya masikini –TASAF na kusema kuwa zile changamoto za walengwa kutoonekana kwenye Orodha zitaisha.