Chai FM

Jamii yatakiwa kutowatenga wagonjwa wa fistula

21 February 2022, 9:45 am

RUNGWE-MBEYA

NA:BETRIDA ANYEGILE

Wito umetolewa kwa jamii wilayani Rungwe mkoani Mbeya kuachana na dhana potofu juu ya ugonjwa wa Fistula kwani ugonjwa huo unatibika bure bila mgonjwa kugharamia gharama yoyote.

Akizungumza kwa njia ya Simu na Chai FM Program manager wa CCBRT Tanzania Bw. Clement Ndahan ametoa rai kwa wanaume kushiriki kikamilifu kulinda afya za wanawake kwa kushirikiana nao bila kuwatenga wagonjwa wa fistula katika maeneo yao.

 

Awali Chai FM imefanya mazungumzo na  Nuru Amosi ambaye alipata tatizo la fistula kabla ya kpata matibabu ambapo ameeleza kwamba jamii ilimtenga ikiwa ni pamoja na yeye binafsi kujinyanyapaa.

Nuru Amosi akitabasam baada ya kutibiwa tatizo la Fistula lililomtesa kwa mwaka na miezi sita.

Aidha Bi. Nuru anatoa rai kwa wanawake na jamii kwa ujumla kutoficha maradhi yanayowasumbua badala yake wajioneshe kwa jamii ili kupatiwa msaada wa matibabu kama ilivyokuwa kwake.

Bi Joyce Mwakang’ata ni balozi wa Fistula katika wilaya za Rungwe, Kyela na Ileje amewataka wanawake kuhudhuria kliniki mara tu wanapojisikia wajawazito huku akisisitiza wanawake kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya kwani itasaidia kupunguza tatizo la Fistula kwa jamii.

Balozi wa fistula wilaya za Rungwe, Kyela na Ileje Bi. Joyce Mwakang’ata kulia akimpongeza Nuru baada ya kurejea nyumbani akitokea CCBRT kupatiwa matibabu.

Huduma za afya za kutibu ugonjwa huu ni bure katika baadhi ya hospitali nchini Tanzania ikiwemo CCBRT, lakini kukosa elimu kwa baadhi ya wanawake husababisha matibabu kutowafikia kwa wakati.