Chai FM

Umbali chazo cha unyanyasaji wilayani Rungwe

24 December 2021, 5:45 am

Umbali wa malezi uliopo baina ya wazazi, walezi, walimu na watoto imetajwa kuwa moja kati ya sababu zinazopelekea kushamiri kwa vitendo vya unyanyasaji dhidi ya watoto wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Aidha jamii imetakiwa kuwalinda zaidi watoto huku wazazi wakitakiwa kujenga urafiki zaidi na watoto ili kubaini changamoto zinazowakabili watoto katika mazingira yanayowazunguka.

Hayo yameelezwa na mratibu wa mafunzo ya stadi za maisha yanayofadhiliwa na shirika la kuwahudumia watoto ulimwenguni UNICEF kwa walimu wa shule za msingi na sekondari wilayani hapa Mwl. Michael Malecela ambapo amesema kwamba ni jukumu la jamii na wazazi kuwajengea watoto wao uwezo wa kujiamini na kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia shuleni.

Mratibu wa mafunzo hayo Mwl. Michael Malechea akizungumza na washiriki wa mafunzo hawapo pichani.

Mwl. Yona Mwaisaka ni afisa elimu sekondari wilayani hapa akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi mkurugenzi wa halamshauri amewataka walimu kuyatumia mafunzo hayo kwa ufanisi ili kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi kama vile mimba za utotoni pamoja na utoro, huku akisisityiza walimu kutumia taaluma kumuadabisha mwanafunzi badala ya viboko.

Mwl. Yona Mwaisaka afisa elimu sekondari wilayani Rungwe akihutubia wakati wa kufunga mafunzo hayo

Steven Mgimba ni mkuu wa chuo cha ualimu mpuguso ametoa rai kwa walimu kuwafundisha wanafunzi na kuwajengea ari ya kutamani kuwa walimu kwani serikali ya Tanzani hadi sasa imejenga vyuo 35 kwaajili ya kuwaandaa walimu wa taifa hili.

Baadhi ya walimu waliohudhuria mafunzo hayo wameishukuru serikali kwa kushirikiana na UNICEF kuandaa mafunzo hayo yatakayo saidia kupunguza changamoto zinazowakabili watoto kama vile ukatili wa kijinsia na utoro.

washiriki wa mafunzo wakimsikiliza kwa makini Mgeni rasmi, hayupo pichani

Mafunzo ya stadi za maisha katika wilaya ya Rungwe yamefanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 20 hadi 22 disemba 2021 katika chuo cha ulimu Mpuguso na kuwakutanisha walimu zaidi ya 200 wa shule za msingi, sekondari na wakuu wa shule zote wilani hapa.