Sibuka FM

Bariadi: Chifu wa Kilulu jela miaka 20, viboko 12 kwa kumiliki fisi

13 March 2025, 1:04 pm

Muonekano wa nje wa jengo la mahakama ya wilaya ya Bariadi ambapo kumefanyika hukumu ya Chifu wa Kilulu aliyekuwa anamiliki nyara za serikali bila kuwa na kibali Picha kutoka maktaba ya Sibuka fm

Je sheria zetu zinasemaje mtu mpaka kuanza kumiliki nyara za serikali bila kuwa na kibali chochote kutoka kwa mamlaka za uhifadhi wanyamapori huyo mnyama mpaka anaanza kumilikiwa je ! mamlaka za uhifadhi tulikuwa wapi kuzuia vitendo hivyo ni fikra zangu tu”.

Na, Daniel Manyanga

Mahakama  ya wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu imemuhukumu kifungo cha miaka 20 jela sambamba na kuchapwa viboko 12 Emmanuel John mwenye miaka 31 maarufu kwa jina la  Chifu wa Kilulu kwa kosa la kukutwa na nyara ya serikali nyumbani kwake bila kuwa na kibali cha umiliki wa nyara hiyo.

Mbele hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Bariadi, Mhe.Caroline Kiliwa mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya mashtaka ya Taifa mkoa wa Simiyu,Lupiana Mahenge ameiambia mahakama hiyo kuwa mshtakiwa huyo ni mkazi wa  Kilulu  kata ya Bunhamala halmashauri ya mji wa  Bariadi ambaye pia ni  mganga wa kienyeji alikutwa na fisi huyo akiwa hai nyumbani kwake bila ya kuwa na kibali chochote cha uhalali wa kumiliki nyara hiyo.

Lupiana Mahenge amesemaa kuwa mnamo Januari 01, 2025 katika eneo la Kilulu mtuhumiwa alikamatwa kufuatia jeshi la polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema ambao walitoa taarifa kuhusu mtuhumiwa kuishi na fisi hai ndani kwake na kufanikisha kukamatwa kwake

Mwendesha mashtaka huyo kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka mkoa wa Simiyu amesema kuwa kutokana na kosa la kumiliki nyara za serikali bila kuwa na kibali ni kinyume na kifungu cha 86 (1)  (2) (C) (III) cha sheria ya uhifadhi wanyamapori sura ya 283 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Kifungu hicho kinasomwa kwa pamoja na haya ya 14, jedawali la kwanza na kifungu cha 57 (1) na kifungu cha 60 (2) cha sheria ya kupambana na uhujumu uchumi sura ya 200 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Upande wa mashitaka katika kuthibitisha kosa hilo ulipeleka mahakamani mashahidi sita ambao waliithibitishia mahakama pasina kuacha shaka kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo la kumiliki nyara za serikali bila kuwa na kibali chochote kutoka kwa mamlaka za uhifadhi wanyamapori ndipo upande wa mashtaka ukaomba mshitakiwa apewe adhabu kali ili iwe funzo kwake na watu wengine wenye tabia za kumiliki nyara za serikali bila kuwa na kibali chochote kutoka kwa mamlaka ya uhifadhi.

Mtuhumiwa alipopewa nafasi ya kujitetea aliomba mahakama hiyo imsamehe kwa kuwa anategemewa na familia ya watoto wanne wakiwemo watoto mapacha lakini pia ni kosa lake la kwanza na hakukusudia kumiliki nyara za serikali bila kuwa na kibali chochote kutoka kwa mamlaka za uhifadhi wanyamapori.

Akitoa hukumu hiyo hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Bariadi Mhe. Caroline Kiliwa amesema kuwa mahakama hiyo imejiridhisha bila kuacha shaka yoyote kuwa, Emmanuel John jina maarufu Chifu ametenda kosa huku alikuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria ndipo akamhukumu kwenda kutumikia adhabu ya miaka 20 jela na kuchapwa viboko 12 na ataanza kutumikia adhabu hiyo kuanzia siku ya hukumu mnamo tarehe 12.03.2025.