

12 March 2025, 12:19 pm
“Hatuwezi kuendelea kuona watu ambao wanapambana katika kujikwamua kiuchumi kwa kufanya shughuli mbalimbali wanarudishwa nyuma na watu ambao hawana nia njema ya kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja hadi Taifa kwa ujumla lazima tuwajibishane kwa kufuata sheria ili kukomesha tabia hizo “.
Na, Daniel Manyanga
Mahakama ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imewahukumu washtakiwa wawili kwenda jela miaka mitano Kila mmoja baada ya kukutwa na kesi ya wizi wa mnyama Nguruwe hukumu iliyotolewa Jumanne tarehe 11.03.2025 mahakama hapo.
Mbele hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya ya Maswa,Mhe.Aziz Khamis mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka wilayani hapo mkaguzi msaidizi wa polisi ,Vedastus Wajanga amewata kwa majina washtakiwa hao Masunga Chenya (20) na Daud Elias (19) wakazi wa mtaa wa Sola mjini Maswa.
Mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka wilaya hiyo, Mkaguzi Msaidizi wa polisi, Vedastus Wajanga aliieleza mahakama kuwa kwa pamoja waliiba Nguruwe mmoja mwenye thamani ya Tsh.500,000 mali ya Clerdes Donacian mkazi wa mtaa wa Sola wilayani humo.
Vedastus Wajanga amesema kuwa tukio hilo lilitokea mwezi Septemba 2,2024 majira ya saa 11:00 alfajiri mara baada ya washitakiwa wote kuingia ndani ya zizi la Nguruwe linalomilikiwa na Clerdes Donacian na kuiba Nguruwe huyo ambaye ni dume na siku hiyo hiyo walikamatwa wakiwa naye katika mtaa huo wa Sola.
Taarifa zilifika kituo cha polisi wilaya hiyo na askari polisi wafika eneo la tukio nakukuta tayari washtakiwa wapo chini ulinzi wa wananchi wakiwa pamoja na kielelezo ambacho ni nguruwe.
Katika kesi hiyo Namba 31726/2024 walishtakiwa katika mahakama hiyo kwa makosa mawili la kwanza ni wizi wa mifugo kinyume na kifungu cha 258 (1)(2) (a) na 268 (1)(3)cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022 .
Na kosa la pili la kupatikana na mali idhaniwayo kuwa ni ya wizi kinyume na kifungu cha 312(1)(b) na( 2) Cha sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022.
Upande wa mashitaka ulileta jumla ya mashahidi watano na vielelezo viwili ambavyo vilitolewa mahakamani hapo ili kuthibitisha makosa waliyoyafanya washitakiwa.
Mara baada ya washtakiwa kutiwa hatiani upande wa mashtaka uliiomba mahakama kuwapatia adhabu kali ili iwe funzo kwao na kwa jamii kwani matuko ya wizi wa mifugo yanaongezeka ndani ya wilaya hiyo na mkoa huo.
Amesema kuwa washitakiwa ni vijana ambao wana nguvu za kuweza kufanya kazi nakujipatia kipato halali na pia vitendo hivyo vya wizi vinadidimiza kipacho cha mwenye mali na huweza kusabisha wananchi kujichukulia sheria mkoni na hatimae kusababisha mauaji.
Akitoa hukumu hiyo hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya ya Maswa,Mhe.Aziz Khamis amesema kuwa mahakama imejilidhisha bila kuacha shaka yoyote kuwa washtakiwa wote walitenda kosa hilo huku wakijuwa kuwa kufanya hivyo ni kosa la jinai hivyo wanaenda kutumikia kifungo cha miaka mitano kila mmoja.