

2 March 2025, 11:16 am
Malengo ya kuanzishwa kwa Mnada huo ni kusogeza huduma kwa Ukaribu ya uuzaji wa Mifugo, Upatikanaji wa Mahitaji mbalimbali ya kila siku kwa Wananchi wa Wigelekelo na maeneo jirani pamoja na kuongeza wigo wa Ukusanyaji wa Mapato katika Halmashauri
Na ; Nicholaus Machunda
Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu imezindua Mnada Mpya utakaosaidia kuongeza Mapato ya Halmashauri na kusogeza Huduma kwa wananchi wa kijiji cha Wigelekelo na Maeneo jirani yanayozunguka mnada huo.
Akizungumza wakati kuzindua Mnada huo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Maswa Dkt Vicent Naano Anney, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Athumani Zahoro Kalaghe amewapongeza Madiwani na Wataalam kwa ubunifu wa Mnada huo ambao utaenda kupanua wigo wa huduma kwa wananchi na kuongeza mapato
Kalaghe ametoa rai kwa wananchi wa Maswa na Maeneo jirani kujitokeza kuchukua Vizimba kwa ajili ya Biashara bure huku akitoa maagizo kwa Mkurugenzi kuhakikisha wanaboresha miundo mbinu katika Mnada huo ili iwe rafiki kwa wafanyabiashara.
Akitoa taarifa kwa Mgeni rasmi, Mkuu wa Divisioni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Robert Urassa amesema kuwa malengo ya uanzisha mnada ni kufikisha kwa ukaribu uuzaji wa Mifugo pamoja na kusogeza huduma kwa Wananchi ili kurahisisha kupata Mahitaji ya nyumbani ya kila siku
Paul Maige ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ameeleza mchakato wa kuanzisha mnada mpya katika kijiji cha Wigelekelo kata ya Masela huku akiwatoa wasi wasi wananchi kuhusu uwakilishi wa Wananchi katika Baraza la Madiwani
Akitoa salamu za Chama, Mwenyekiti wa ccm wilaya ya Maswa Onesmo Makota amewapongeza wote walioshiriki kufanikisha wazo la uanzishwaji mnada huo kwani ndio malengo mahususi ya Chama cha Mapinduzi ya kusogeza huduma kwa Wananchi
Diwani wa Kata ya Masela Mhe Kulwa Gwisu Hinda amesema kuwa aliwasilisha kama wazo la kuanzisha mnada kwenye Baraza la Madiwani ili kuongeza mapato na wazo hilo likaboreshwa na Wataalamu wa Halmashauri na kuanza utekelezaji hatimae kukamilika na wananchi kuanza kupata huduma na mahitaji mbalimbali
Baadhi ya Wananchi na Wafanya biashara walioshiriki Uzinduzi wa Mnada Mpya huo wameipongeza Halmashauri kwa Ubunifu huko wa kusogeza huduma kwa Wananchi huku wakiomba uboreshaji wa Miundo mbinu katika eneo hilo na wananchi waendelee kuhamasishwa kupeleka biashara zao