Idadi ya watalii wa ndani imeshuka pori la akiba Kijereshi
8 January 2025, 8:05 pm
“Elimu ya utalii bado inahitajika kwa jamii ili kuwajengea uzoefu wa kupenda kutembelea vivutio mbalimbali kwa lengo la kujifunza pamoja na kuchangia pato la Taifa”.
Na, Daniel Manyanga
Imeelezwa kuwa elimu utalii bado inahitajika kwa wananchi mkoani Simiyu ili waweze kuhamasika kutembelea maeneo mbalimbali yenye vivutio na kufanya utalii wa ndani hivyo kuchangia pato la serikali kwa maendeleo Taifa kwa ujumla.
Wakizungumza na Sibuka fm baadhi ya viongozi wa maeneo yanayozunguka pori la akiba Kijereshi walipotembelea katika pori hilo kwa ajili ya kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo katika pori hilo sambamba na kuhamasisha utalii wa ndani, ambapo wameeleza kuwa upo umuhimu mkubwa wa kuendelea kuielimisha jamii juu ya kufanya utalii wa ndani pamoja na kutangaza vivutio hivyo.
Kwa upande wake afisa mhifadhi mwandamizi wa pori la akiba la Kijereshi kutoka mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania (TAWA) Rogathe Wado amesema kuwa mwitikio wa watalii wa ndani katika pori hilo bado ni mdogo hivyo kuna kila haja ya kuendelea kutoa elimu ya utalii kwa wananchi.