World Vision yawapiga msasa wajumbe wa kamati ya maafa Maswa
16 September 2024, 7:00 pm
“Katika kukabiliana na maafa mbalimbali hapa nchini shirika lisilo la kiserikali la World vision limeendesha mafunzo kwa kamati za maafa ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji wakati ,kabla na baada ya maafa”.
Na, Daniel Manyanga
Kamati za Maafa za wilaya zimetakiwa kuandaa miongozo ya kupambana na maafa ili kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao una kuwepo wakati majanga yanapotokea pamoja na kuhakikisha zinafanya maandalizi ya kutosha ya kukabiliana na maafa ili kuinusuru jamii ilikumbwa na changamoto hiyo.
Wito huo umetolewa na naibu waziri,ofisi ya waziri mkuu (Sera, Uratibu na Bunge),Mhe.Ummy Nderiananga wakati akifungua mafunzo kwa kamati ya maafa ya wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu yaliyofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya na kuhudhuriwa na wajumbe wa kamati ya maafa wilayani hapo.
Naibu waziri, Nderiananga amesema kuwa miongozo hii inajumuisha mikakati mbalimbali ambayo inaweza kufuatwa kabla, wakati, na baada ya maafa kutokea kwani hatua hizi zinahitaji maandalizi mazuri, rasilimali za kutosha,na ushirikiano kati ya taasisi, serikali, na jamii.
Mashimba Ndaki ni Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, amesema kuwa maafa yamekuwa yakitokea kila wakati katika jamii hivyo Kupitia mafunzo hayo ambayo yamewaongezea namna Bora ya kukabiliana na maafa itawafanya wafanye vizuri katika kukabiliana na maafa katika jamii.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge amesema kuwa ofisi ya waziri mkuu imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kukabiliana na maafa pindi yanapotokea hapa nchini hivyo kama wilaya watafanya kazi kwa mjibu wa miongozo ya maafa.
Awali mkurugenzi msaidizi, operesheni na uratibu, idara ya maafa,ofisi ya waziri mkuu, Luteni Kanali,Selestine Masalamado amesema kuwa wameamua kutoa mafunzo hayo kwa kushirikiana na Shirika la World Vision ili kuzijengea uwezo kamati za Maafa za wilaya ziweze kuandaa mikakati ya kupunguza hatari za maafa kwa kuimarisha miundombinu na kutoa elimu kwa jamii juu ya namna ya kuepuka au kupunguza athari za maafa.
Amesema kuwa tayari mafunzo haya yametolewa katika mikoa mbalimbali hapa nchini ikiwemo Tabora na Shinyanga na kwa mkoa wa Simiyu mafunzo hayo yatatolewa katika wilaya za Maswa,Itilima na Meatu.