RC Kihongosi aagiza kurejeshwa fedha za mikopo ya vikundi Maswa
24 June 2024, 12:33 pm
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe, Kenan Kihongozi ameahidi kuunda tume ya kufuatilia urejeshaji wa mikopo ya 10% kwa vikundi vya wanawake, vijana na makundi maalum inayotolewa na halmashauri ili watanzania wengine waweze kukopa.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Kenan Laban Kihongosi amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kuhakikisha wote waliochukua Mikopo ya Asilimia Kumi (10%) inayotolewa kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Makundi Maalumu warudishe ili Watanzania wengine waweze kukopa.
Mhe Kihongosi ametoa maagizo hayo Wilayani Maswa wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani la kujadili Hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali ( CAG ) na kusema kuwa ataunda tume maalumu kwa ajili ya kufuatilia urejeshaji wa Mikopo hiyo ili ziweze kunufaisha wengine
Aidha Mkuu wa Mkoa ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kwa kupata HATI Safi ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali huku akiwata kuwachukulia hatua wote waliosababisha Hoja kwa Uzembe wa Makusudi ili Watanzania waendelee kuiamini Serikali yao.
Akitoa taarifa za Ukaguzi wa Hesabu za Serikali, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo Lwiza Sudi amesema kuwa Hoja iliibuliwa kutokana na Deni la Mkopo wa Asilimia kumi (10% ) unaotolewa kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu kutorejeshwa.
Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe, Aswege Kaminyoge amesema kuwa anamshukuru Rais Samia kwa kutoa Fedha nyingi kwa ajili ya Miradi mbalimbali ya Maendeleo kwa Wananchi wa Maswa .
Jeremia Shigala na Aron Mboje ni Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa wamemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuwapitisha vyema katika Hoja za CAG na kuahidi kuyasimamia na kuyafanyika kazi ili Halmashauri iendelee kupata HATI safi.