Maji ya sumu mgodini yatishia usalama wa mifugo, wananchi Busega
4 June 2024, 5:43 pm
“Serikali bila watu hakuna utakachokifanya hivyo niseme serikali ni watu ndiyo ni kweli tunahitaji mapato kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini lakini linapokuja suala la afya za wananchi hakuna umuhimu wa madini.”
Na, Daniel Manyanga
Mkuu wa Wilaya ya Busega mkoani Simiyu Faidha Salim amesitisha shughuli za uchenjuaji wa dhahabu katika mgodi wa EMJ uliopo katika kijiji cha Imalamate mpakani mwa wilaya ya Busega na Bariadi kutokana na maji yanayotumika katika shughuli za uchenjuaji yanayodhaniwa kuwa na sumu kuua ng’ombe watano na mbuzi mmoja pamoja na kusababisha madhara kwa wananchi.
Faidha Salim amechukua maamuzi hayo kufuatia ng’ombe watano na mbuzi mmoja kufa na ng’ombe wengine zaidi ya 80 hali zao siyo nzuri kutokana na kunywa maji yanayodhaniwa kuwa na sumu yanayotiririka kutoka mgodini na kwenda katika vyanzo vya maji vilivyopo karibu na mgodi huo.
Faidha Salim amesema kuwa mbali na mifugo kuathiriwa lakini kuna wananchi ambao wameanza kuona madhara mbalimbali kutokana na kutumia maji hayo katika shughuli za kijamii hivyo amelazimika kusitisha shughuli za uchenjuaji wa dhahabu na kupisha uchunguzi wa kimaabara ili kubaini nini chanzo cha vifo vya mifugo hiyo.
Wakizungumza na Sibuka FM baadhi ya wananchi wamesema kuwa kutokana na kuyatumia maji hayo katika matumizi mbalimbali yamewaathiri kiafya hivyo wameomba serikali kuchukua hatua kali dhidi ya mgodi huo ili kunusuru mifugo na wananchi wanaotumia maji katika vyanzo vilivyopo karibu na mgodi.
Kwa upande wake Paul John mwenyekiti wa kijiji cha Imalamate amesema kuwa hadi sasa wafugaji wa eneo hilo wameingiwa na hofu kubwa kutokana na kutokuwa na vyanzo vingi vya kunyweshea mifugo yao kutokana na tishio hilo huku diwani wa kata ya Imalamate, Richard Magoti akiomba serikali kuchukua hatua haraka dhidi ya mgodi huo ili kunusuru madhara zaidi yanayoweza kujitokeza kwa mifugo na wananchi katani hapo.