Roundabout kumaliza ajali za barabarani Lamadi
14 May 2024, 5:30 pm
Barabara ya mzunguko ilichelewa sana kuwepo na huenda ajali za barabarani zisingekuwepo au kuwepo lakini kwa kiwango cha chini tofauti na hivi sasa.
Na, Daniel Manyanga
Kukamilika kwa barabara ya mzunguko (roundabout) inayounganisha barabara za Lamadi Bariadi,Mwanza na Mara kunatajwa kupunguza ajali ambazo zilikuwa zikitokea mara kwa mara kwenye eneo hilo.
Wakizungumza na Sibuka Fm baadhi ya Wakazi hao ,Recho Johashi na Masunga Sospeter wamesema kuwa ajali hizo zilihusisha watembea kwa miguu ikiwemo wanafunzi pamoja na magari kukosea njia hatua iliyopelekea mengine kuanguka lakini kuwepo kwa njia hiyo inaenda kumaliza tatizo hilo.
Kwa upande wake msimamizi wa mradi huo kutoka wakala wa barabara mkoa wa Simiyu (TANROADS ) mhandisi Amri Elias amesema kuwa zaidi ya kiasi cha shilingi milioni mia nane arobaini kinatarajia kutumika kwenye ujenzi wa barabara hiyo ya mzunguko hadi kukamilika kwake.
Amri ameongeza kuwa wakala wa barabara mkoa wa Simiyu (TANROADS) walifikia maamuzi ya kujenga roundabout kutokana na changamoto mbalimbali za barabarani zinazotokea maeneo hayo.