Maswa kuvuna pamba chini ya lengo
17 May 2024, 11:56 am
Kutokana na mvua kuwa kubwa kunyesha msimu huu wa kilimo kwa mwaka 2023/2024 zilizopelekea mavuno ya pamba kushuka wilaya ya Maswa inatarajia kukusanya mapato chini ya makadirio ya awali.
Na, Daniel Manyanga
Zaidi ya tani elfu ishirini na mbili za zao la pamba zinatarajiwa kuvunwa wilayani Maswa mkoani Simiyu katika msimu wa ununuzi wa zao hilo kwa mwaka 2024/2025 kutoka kwenye malengo ya awali ya kuvuna tani zaidi sitini elfu wilayani hapo.
Akizungumza na Sibuka Fm mara baada ya kuzinduliwa kwa msimu wa ununuzi wa zao la pamba wilayani hapo mkuu wa divisheni ya kilimo,mifugo na uvuvi wilaya, Robert Urasa amesema kuwa kutokana na mvua kuwa kubwa msimu huu mavuno yanatarajiwa kushuka hadi kufikia tani ishirini na mbili elfu kutoka makadirio ya awali ya kuvuna tani zaidi ya sitini elfu.
Urasa ameongeza kuwa kutokana na changamoto hiyo kujitokeza katika msimu huu tayari wilaya imeanza kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa pamba kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2024/2025 ili halmashauri ya wilaya iweze kupata kodi itokanayo na ununuzi wa pamba.
Awali mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge akifungua rasmi msimu wa ununuzi wa pamba amesema kuwa kabla ya kuanza kununua watakaa kwa pamoja na wadau wa pamba ili kuweka mpango mkakati wa kukusanya pamba bila ya kuacha madeni kutoka kwa makampuni,AMCOS na wakulima pindi msimu wa ununuzi unapomalizika.
Kwa upande wake meneja wa chama kikuu cha ushirika mkoa wa Simiyu (SIMCU) Falesi Muganda amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa AMCOS ya kuwaibia wakulima pindi wanapoenda kuuza pamba kwa kubana mizani ili wao waweze kupata faida badala ya wakulima kuacha mara moja hiyo tabia.