Mvua yageuka kilio kwa wakulima wa pamba Bariadi
29 April 2024, 5:41 pm
Licha ya mvua kuwa na faida lakini kwa wakulima wa pamba Bariadi imegeuka kilio hadi kufikiria kulima mazao mengine ili kujikomboa kiuchumi kutokana na mavuno ya pamba kuwa chini msimu huu.
Na, Daniel Manyanga
Wakulima wa zao la pamba halmashauri ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu wamelia na mvua inayoendelea kunyesha kuharibu zao hilo hatua itakayopelekea uzalishaji kushuka na hivyo kutokufikia malengo yao katika msimu huu wa kilimo cha zao hilo.
Wakizungumza na Sibuka FM kwa nyakati tofauti, Daud Mashimo na Nkuhi Simiyu wamesema kuwa kutokana na mvua kuwa kubwa mavuno yatashuka kutokana na zao hilo kutohitaji mvua za juu ya wastani ambapo kwa hekari moja walitarajia kupata tani moja ambapo kwa sasa wanaweza kupata labda 200kg kutokana na mashamba kujaa maji.
Issa Mtweve ni Mkuu wa Idara ya Kilimo na Uvuvi halmashauri ya mji wa Bariadi amekiri uwepo wa changamoto hiyo ambayo inaenda kupunguza kiwango cha uzalishaji wa zao hivyo kushuka kwa asilimia 25.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bariadi,Simon Simalenga amesema kuwa maeneo ya bondeni ndiyo yameathiriwa na wingi wa mvua hivyo kuleta changamoto kwenye uzalishaji kwa msimu huu kutokana na mvua kuzidi.
Katika hatua nyingine Simon Simalenga amewataka wakulima wawe wabunifu kwa kulima mazao mengine kutokana na mvua hizi zinazoendelea kunyesha ili kuweza kujikomboa.