Homa ya mapafu yatishia usalama wa mifugo Maswa
23 April 2024, 8:58 am
Zoezi la uchanjaji wa mifugo wilayani Maswa mkoani Simiyu kuwasaidia wafugaji kufanya ufugaji wenye tija na kuongeza thamani ya mifugo yao hivyo kuondokana na umasikini.
Na,Paul Yohana
Zaidi ya ng’ombe laki tatu wilayani Maswa mkoani Simiyu kupatiwa chanjo ya homa ya mapafu ili kukabiliana na ugonjwa huo ambao unaenea kwa kasi hali inayopelekea kufungwa kwa baadhi ya minada na kuwatia umasikini wafugaji.
Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Maswa, Paulo Maige wakati wa uzinduzi wa zoezi la utoaji wa chanjo ya homa ya mapafu kwa ng’ombe lililofanyika kijiji cha Mwanh’egele kata ya Nyabubinza wilayani hapo.
Samwel Nyalandu ni katibu wa chama cha wafugaji wilayani hapo amesema kuwa wafugaji wanakabiliwa na changamoto za malisho,maji na masoko huku akiwaomba wafugaji kujiunga na chama hicho ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na benki bila kuwa na mashariti magumu.
Kwa upande wake daktari wa mifugo wilaya hapo Dkt.Charles Masila akisoma ripoti mbele ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo amesema kuwa wamekusudia kuchanja ng’ombe zaidi ya laki tatu ili kuweza kuikinga mifugo na homa ya mapafu ambao umeonekana kukua na kusambaa kwa kasi na kusababisha vifo kwa mifugo hali inayosababisha kufungwa kwa baadhi ya minada.
Akizungumza kwa niaba ya wafugaji, Malale Mbizo amesema kuwa serikali inapaswa kuendelea kutoa chanjo hizo ili kuikinga mifugo na magonjwa kama hayo.