Sibuka FM

Mchungaji awa mpiga ramli chonganishi kwa waumini wake Maswa

2 October 2024, 3:33 pm

Pichani aliyesimama ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi akizungumza na wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero na kuzitafutia ufumbuzi. Picha na Nicholaus Machunda

“Watu kwenda kanisani kuombewa kutokana na changamoto zao siyo dhambi lakini hatuwezi kuwafumbia macho baadhi ya watumishi wa Mungu ambao wanageuka kuwa wachonganishi kama na wao waganga wa kienyeji ambao wanatumia ramli chonganishi, twendeni tukafanye kazi ya Mungu na siyo vinginevyo.”

Na,Daniel Manyanga

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ameagiza kuchunguza na kufuatilia huduma zinazotolewa na Kanisa la International Evangelical Assembles of God Tanzania (IEAGT) lililopo kata ya Shishiyu wilayani Maswa kufuatia tuhuma za kuendesha ibada chonganishi.

RC Kihongosi ametoa maagizo hayo kwa Mkuu wa Wilaya ya Maswa Aswege Kaminyoge wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Shishiyu akiwa ziarani wilayani hapo, ziara yenye lengo la kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

Mkuu huyo wa Mkoa amemwagiza mchungaji huyo kuhakikisha mapepo hayo hayataji tena majina ya wakazi wa eneo hilo kwa kuwa ibada hiyo inaleta taharuki kwa wananchi hao.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Kenani Kihongosi akitoa maelekezo kwa mchungaji anayetuhumiwa kutumia dini kuchonganisha wananchi

Akizungumzia tuhuma hizo mchungaji wa kanisa hilo, Mch. Joseph Jackson amesema kuwa yeye hajamtuhumu mtu yeyote kuwa ni mchawi isipokuwa ni waumini wanaofika kanisani hapo kufanyiwa maombi mapepo yakipanda ndipo hutaja majina ya wachawi hao.

Sauti ya mchungaji Joseph Jackson akikanusha tuhuma za kuchonganisha wananchi katika kata hiyo.

Awali akitoa malalamiko kwa Mkuu wa Mkoa,  Bi. Pili Abrahiman Kidesela mkazi wa kata ya Shishiyu wilayani hapo amesema kuwa mchungaji huyo amekuwa kero kwa wakazi wa eneo hilo kwa kuendesha ibada zinazowatuhumu wakazi wa eneo hilo kuwa ni wachawi.

Akizungumza na Sibuka FM, Bi.Lucia Marko amesema kuwa yeye ni mhanga wa mafundisho ya mchungaji huyo kwa kuwa alitajwa na kutuhumiwa kuwa  ni mchawi na huwa anaenda kwenye kanisa hilo kuliwangia.

Sauti ya wananchi wakitoa malalamiko mbele ya Mkuu wa Mkoa kufuatia kutuhumiwa kuwa ni wachawi

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Maswa Aswege Kaminyoge amesema kuwa suala la mchungaji huyo analitambua na alishakutana naye wakati wa zoezi la kudhibiti kipindupindu kilipozuka na kumtaka mchungaji huyo kusitisha mikusanyiko lakini hakuwa tayari hivyo watahakikisha wanalifanyia kazi kwa weledi ili kuondoa sintofahamu kwa jamii hiyo.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge akizungumzia uwepo wa taarifa za mchungaji huyo.