TVS 150 kupeleka kicheko kwa wateja wa maji mjini Maswa
15 July 2024, 9:10 pm
“Katika kurahisisha wananchi wanapata maji safi na salama wakati wote mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Maswa MAUWASA imepokea vifaa vya usafiri ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji”
Na, Daniel Manyanga
Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Maswa (MAUWASA) wilayani Maswa mkoani Simiyu imepokea Pikipiki 8 zikiwemo aina ya TVS 150 ili kuboresha huduma za maji kwa wateja na kuongeza ufanisi wa kiutendaji.
Akipokea pikipiki hizo mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Maswa (MAUWASA), Mhandisi Nandi Mathias ameishukuru serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania chini ya Rais,Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pikipiki hizo ambazo zinaenda kuboresha huduma za maji na kuleta ufanisi wa kiutendaji mjini Maswa pamoja na vijiji 20 vinavyopata huduma ya maji kutoka MAUWASA.
Nao baadhi ya watumishi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Maswa (MAUWASA), Queen Mlagala na Samson Makulu wamesema kuwa Pikipiki hizo zitasidia utendaji wa kazi na kuleta ufanisi hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji pamoja za kuzuia mivujo ya maji mjini na vijiji ambavyo vinapata huduma ya maji kutoka MAUWASA.
Katika hatua nyingine ,Mhandisi Nandi Mathias ametoa rai kwa wananchi wanaojiunganishia huduma ya maji safi na salama bila kufuata taratibu za kupata huduma hiyo kuacha mara moja kwani ni kosa kisheria hivyo wananchi wafuate utaratibu wa kupata huduma hizo.